KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, January 6, 2011

Viongozi CHADEMA waachiwa kwa dhamana


Wanachama 31 wa chama cha upinzani CHADEMA nchini Tanzania kati ya 49 waliokamatwa kutokana na ghasia baina ya wananchi na polisi wamesomewa mashtaka mahakama kuu mjini Arusha.

Waliobaki 18 miongoni mwa 49 walikutwa hawana hatia na kuachiliwa.

Hata hivyo wanachama hao 31 huku 10 wakiwa viongozi wa CHADEMA wamesomewa shitaka moja la kufanya maandamano kinyume cha sheria na kuachiwa huru kwa dhamana.

Kulingana na mwandishi wa Arusha Ali Shemdoe Kamanda wa polisi mjini humo Tobias Andengenye alisema kufuatia vurugu hizo watu wawili walifariki dunia, kutokana na majeraha waliyoyapata kutokana na mapambano hayo.

Mbali na vifo hivyo pia kumekuwepo na majeruhi 11 wakiwemo polisi wawili.

Anayejulikana kuwa mchumba wa Dr Slaa alijeruhiwa na hivyo ilibidi mahakama ikamsomee mashtaka yake katika hospitali ya Mount Meru mjini humo ambapo alikuwa akiendelea kupata matibabu.

Mbali na hayo uharibifu mkubwa umefanyika hasa kwenye jengo la mfanyabiashara maarufu mjini humo na pia kwenye vituo viwili vya polisi.

Shemdoe alisema hali ya usalama imekuwa shwari mjini humo, na watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Vile vile alisema kumekuwa na hisia tofauti kuhusiana na vurugu hizo huku wengine wakiona sawa kwa polisi kutumia nguvu japo wengine wakisema polisi hawakustahili, na walifanya kosa.

No comments:

Post a Comment