KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Mzee Huyu Balaa!


Asubuhi huonekana mitaa ya katikati ya jiji la Dar es Salaam akijifanya mlemavu wa miguu akiomba omba, jioni huonekana kweye kumbi za starehe akipata ulabu.
Mzee mmoja ambaye kwa muda mwingi amekuwa akiishi kwa shughuli za kuombaomba katikati ya jiji la Dar es Salaam , amekuwa gumzo jijini kwani inasadikika kuwa mzee huyo anamiliki nyumba yake huko Kigamboni na imekuwa ni desturi yake ya kuomba ambapo amekuwa akijifanya mlemavu kumbe siyo mlemavu.

Mzee huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 50 na 60 amekuwa akikaa kwa staili ya aina yake katika makutano ya barabara ya Azikiwe na Samora mbele ya jengo la IPS.

Ikifika tu majira ya saa nne utamkuta eneo hilo na ukaaji wake hukalia matako huku miguu yake akiikunjia kwa ndani hivyo wasamaria wema wamekuwa wakimsaidia pesa nyingi wakidhani kuwa ni mlemavu kumbe ni danganya toto.

Baadhi ya watu tayari wameshaanza kumgundua na kuacha kumsaidia kwani hata wenzake wenye ulemavu wa kweli wamekuwa wakinyimwa msaada kwa madai kuwa wanajifanyisha.

Kali ya yote mzee huyo akiishajikusanyia pesa za kuombaomba jioni yake huenda kulewa katika vilabu vya starehe.

Hivi karibuni gazeti moja la kila siku la Tanzania Daima lilichapisha picha zake zilizoonyesha akitembea kwa miguu yake bila ulemavu pia nyingine zikimuonyesha akigida bia kwa raha zake.

Mbali ya maisha yake ya kuponda mali, mzee huyo pia inasemekana amejenga nyumba kwa kuomba kuomba katika maeneo ya Kigamboni.

Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojigeuza omba omba na kujifanya wana ulemavu ili mradi waweze kujikusanyia pesa kilaini.

Kwa upande mwingine ongezeko la watoto ombaomba limezidi kushamiri nchini hasa ukipita barabara ya Bibi Titi Mohamed eneo la Taasisi ya Eimu ya Watu wazima utakuta jioni na asubuhi wamejilaza katikati ya barabara huku wakiwa wameanika nguo zao kana kwamba ni nyumbani kwao.

"Mgambo wa jiji na Halmashauri za jiji wameshindwa kudhibiti hali hii lakini wamekuwa wakikimbilia kuwaharibia mali zao wafanyabiashara za matunda wakidai wao ndio wanachafua jiji", alisema mmoja wa wakazi wa jijini la Dar es Salaam aliyehojiwa na Nifahamishe kuhusiana na omba omba jijini.

No comments:

Post a Comment