KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Mawaziri Tunisia wajitoa chama cha RCD

Televisheni ya taifa imeripoti, mawaziri wote katika serikali ya mpito ya Tunisia ambao walikuwa katika chama cha Rais aliyekimbia, RCD, wamejitoa kwenye chama hicho.

Hata hivyo, mawaziri hao wataendelea kushikilia nafasi zao za uwaziri katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Hapo awali, ilitangazwa kuwa zaidi ya wanachama 30 wa familia ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo walikamatwa

Maandamano Tunisia


Wakati hali Tunisia ikizidi kuwa tete, majeshi yalifyatua risasi za kutoa tahadhari wakati waandamanaji walipoendelea kuzunguka mjini Tunis.

Taarifa kutoka eneo hilo zinaeleza kwamba baadhi ya waandamanaji walijaribu kupanda ukuta wa makao makuu ya RCD.

Majaji wa Tunisia nao waliandamana Tunis wakitaka majaji wote waliofanya kazi chini ya Rais aliyekimbia wajiuzulu.

Vile vile kumekuwa na taarifa za kuwepo maandamano siku ya Alhamis katika miji ya Gafsa na Kef.

Rais Zine al-Abidine Ben Ali alikimbilia Saudi Arabia wiki iliyopita baada ya kufanyika maandamano makubwa ya kupinga ukosefu wa ajira, umaskini na rushwa.

Licha ya kuondoka, maandamano yamekuwa yakiendelea, huku waandamanji wakitaka wanachama wote wa RCD waondoshwe madarakani.

Mawaziri wanne kutoka upinzani wameng'atuka kutoka baraza la mawaziri la serikali ya mpito siku moja baada ya kuundwa, wakitaka mawaziri kutoka chama cha RCD wasihusishwe.

Waziri mkuu Mohammed Ghannouchi na Rais wa serikali ya mpito Fouad Mebazaa- aliyekuwa spika wa bunge dogo- nao wamejiondoa kwenye chama cha RCD ili kujaribu kujiweka mbali na Bw Ben Ali.

No comments:

Post a Comment