KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Lindeni makandarasi wa ndani - Mwakyembe


Elizabeth Ernest
WAKALA wa Ujenzi wa barabara nchini (TANROADS) , imetakiwa kuepuka masharti ya zabuni za ujenzi yenye mwelekeo bayana wa kuwaengua makandarasi wa ndani.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Harrison Mwakyembe jana Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa Chama cha Makandarasi Tanzania (CATA), ambapo alijibu malalamiko makandarasi hao kwamba karibu 60% ya miradi yote ya ujenzi hufanywa na Makandarasi wa nje.

Pia aliwataka Tanroads kuangalia upya viwango vya zabuni wanavyotoa wakati wa kutangaza tenda ili kuwapa fursa makandarasi wa ndani kushiriki nafasi hiyo.

“Sina tatizo na miradi inayotekelezwa na nchini kwa ufadhili wa wabia wetu wa maendeleo, ila tatizon langu ni miradi inayogharamiwa na serikali ya Tanzania,”alisema na kuongeza:

“Haingii akilini kwa miradi hii inayogharamiwa na serikali kutokana na kodi ya wananchi kuendelea kutekelezwa na makandarasi wa nje kwa asilimia 100 bila ushiriki wa makandarasi wa ndani kutokana na sababu kuu tatu”.

Alizitaja sababu hizo ni kutokana na udhaifu wa sarafu ya Tanzania na kwamba mara zote malipo ya makandarasi wa nje hufanyiwa kwa dola badala ya shilingi ya Kitanzania na hivyo malipo yao huwa ni fedha nyingi zaidi na kufanya ujenzi wa barabara nchini kuwa ghali.

Pia mikataba ya Tanzania haiwafungi makandarasi wa nje kuwekeza tunayowalipa nchini na kwamba sehemu kubwa ya malipo yanayofanywa huneemesha uchumi wa nchi nyingine pamoja na kutoa fursa kwa wageni badala ya wananchi wetu.

“Kwakuwa mchakato wa zabuni ni zoezi la kitaalam, makandarasi wa ndani wajitahidi kuajiri watu wenye ujuzi katika masuala ya manunuzi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindani,” alisema.

Katika risala yake Mwenyekiti wa CATA, Mhandisi Lawrence Mwakyambiki alisema anasikitika kuwa bado kuna idara au Taasisi za serikali ambazo hupendelea kwa mazoea kutoa kazi za ujenzi zilizo chini ya bilioni 20 kwa kampuni za nje bila sababu za msingi wakati makandarasi wazalendo wana uwezo wa kuzifanya.

Pia alisema miradi mingi ya serikali imekuwa haifanyiwi matayarisho ya kutosha na washauri pamoja na wataalamu wa serikali pamoja na kutoipa umuhimu unaostahili kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wenyewe

No comments:

Post a Comment