KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Lebanon na mgogoro wa kisiasa

Je ni kweli Hizbollah inahusika na mauaji ya Rafik Hariri?





Kundi la Hezbollah limejiondoa serikalini na kuzusha hali ya wasiwasi ndani na nje ya Lebanon. Jumuiya ya kimataifa imeikosoa hatua hiyo huku Walebanon wakisubiri nani hasa atakamata wadhifa wa Waziri mkuu mpya.

Jumuiya ya nchi za Kiarabu,Arab League imewatolea mwito Walebanon kuwa watulivu baada ya serikali yao ya Umoja wa taifa kuporomoka.Hatua hiyo imefuatia kujiondoa kwa kundi la Hezbollah pamoja na washirika wao kutoka serikali hiyo.Jumuiya ya nchi za kiarabu imeonya kwamba hali inaweza kuzorota ikiwa wanasiasa nchini humo hawatochukua hatua ya kuirudisha tena serikali hiyo.










Kila mwaka watu hukusanyika kuomboleza kifo cha Rafik Hariri


Kuporomoka kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Lebanon kumeitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa na kuzusha hofu pamoja na Sitofahamu miongoni mwa wakaazi wa taifa hilo.Kumekuweko na hali ya wasiwasi kufuatia ripoti kwamba Mahakama ya Kimataifa inayochunguza kuhusu mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu wa Taifa hilo Rafiq Hariri inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inapanga kuwatia hatiani viongozi wa juu wa kundi la kishia la Hezbollah kuhusiana na mauaji hayo yaliyotokea mwaka 2005.

Ni wasiwasi huu ndio uliochangia pia kujiondoa serikalini kwa Mawaziri 11 wa kundi hilo pamoja na washirika wake. Katika taarifa ya jumuiya ya nchi za kiarabu ya Arab League,Katibu mkuu wake Amr Moussa amewataka viongozi wote wa kisiasa nchini humo kuonyesha na kuhubiri amani na utulivu pamoja na kuwa tayari kufungua njia ya kufanyika mazungumzo yatakayoumaliza mgogoro huo.







Wasemavyo wachambuzi

Wachambuzi wa mambo wanasema kwamba hatua hii inaweza kuashiria mwanzo kamili wa mvutano juu ya nani ana madaraka ya kusimamia taasisi za serikali. Juu ya hilo mpasuko huo unaweza kuwa pia lengo la kuhakikisha kwamba serikali haifanyi uamuzi wowote wa kumkamata mtu yoyote atakayetolewa warranti wa kukamatwa na mahakama hiyo maalum inayochunguza mauaji ya Hariri


Uamuzi mgumu unamsubiri rais Michel Suleiman


Rais Michel Suleiman atabidi kushauriana na wabunge wote 128 juu ya nani anayestahili kuchukua wadhifa wa waziri mkuu mpya ambaye analazimika kutoka upande wa kundi la madhehebu ya Sunni. Pamoja na kwamba Saad Hariri ndio kiongozi wa Sunni mwenye usemi mkubwa lakini kinachosubiriwa ni kuona ikiwa atateuliwa tena kushikilia wadhifa huo kutokana na kuwepo uhasama mkubwa kati ya kambi yake na kundi la Hezbollah.

Wasiwasi ulioibuka nchini humo kufuatia hali hiyo mpya ya kisiasa umemfanya pia Kamanda wa jeshi nchini humo Generali Jean Qahwaji kutangaza kwamba majeshi yake yameshajiweka tayari kupambana na hali yoyote ya vurugu itakayotokea.Spika wa bunge Nabih Berri ametangaza kwamba mazungumzo ya kuunda serikali mpya yataanza jumatatu mchana.

No comments:

Post a Comment