KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 30, 2010
Waziri Mkuu wa Tanzania amaliza mgogoro
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda amesuluhisha mgogoro uliokuwepo baina ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wahadhiri wa chuo hicho, kuhusu maslahi yao na wamekubali kuingia madarasani kuanzia Jumatatu, Januari 17, 2011.
Akizungumza na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA), Bw Pinda alisema matatizo yaliyojitokeza katika chuo hicho ni mlundikano wa mambo ambayo yamekuwepo siku nyingi, lakini mengi ni ya kiutendaji tu na yanaweza kuisha bila kupoteza muda mwingi.
“Nimeongea na viongozi wa UDOMASA na kuwaahidi kuwa madai yenu ya posho yanaweza kukamilika mwezi wa Februari, nilitaka yaishe mwezi huu lakini kwa taratibu za HAZINA sasa hivi wameshaanza kushughulikia mishahara ya mwezi wa Januari kwa hiyo marekebisho yenu hayawezi kuwahi…wameniahidi mwezi ujao yatakamilika”, alisema huku akishangiliwa.
Amesema amemwita Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua taarifa za mahesabu ya chuo hicho ili kubaini tuhuma zilizojitokeza za watu kulipwa hundi mbili za mishahara, walioacha kazi kuendelea kuwemo kwenye payroll ya mishahara, na wengine kukosekana kabisa kwenye payroll.
Kuhusu madai ya wanafunzi ya matatizo ya maji, Waziri Mkuu alisema amemwagiza Naibu Katibu Mkuu (Fedha) Bw. John Haule, afuatilie uhamisho wa ndani wa fedha katika Wizara ya Maji ili zipatikane sh. bilioni 1.66 zinazohitajiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dodoma (DUWASA) kuchimba visima maeneo ya Ng’ong’ona na Ihumwa ikiwa ni pamoja na kutandaza mabomba hadi chuoni ili kupunguza shida ya maji haraka iwezekanavyo.
Pia alisema katika mipango ya muda mrefu, DUWASA pia wanataraji kupata dola za Marekani milioni 26 ambazo zitatumika kuchimba visima vingine na kujenga matanki yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 12 za maji na hivyo kuondoa kabisa tatizo la maji chuoni hapo. Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idris Kikula alimweleza Bw Pinda, mahitaji halisi ya maji chuoni hapo ni lita milioni 3.5 kwa siku ambazo kati ya hizo, lita milioni 1.5 ni kwa matumizi ya wanafunzi peke yao na lita nyingine milioni mbili ni kwa matumizi ya ujenzi wa majengo unaoendelea chuoni hapo.
Mapema akizungumza na Kamati ya Makatibu Wakuu iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi, mara baada ya kuwasili mjini Dodoma, Waziri Mkuu alielezwa kuna matatizo ya malipo ya posho na mishahara kwa watumishi na wahadhiri wa chuo hicho.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA), Bw. Idd Mwerange alimwahidi Waziri Mkuu watarudi madarasani wakati wakisubiri madai yao yakamilishwe bali aliomba kuwe na uwakilishi wa UDOMASA katika timu ya watu watakaonana na CAG
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment