KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, December 14, 2010

Wanafunzi Ardhi nao waanza mgomo


Ibrahim Yamola na Imakulate Peter
MWAMKO wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kudai haki zao jana ulihamia Chuo Kikuu cha Ardhi ambako wanafunzi wameamua kuanza mgomo wakishinikiza serikali kumaliza kero kumi ikiwa ni pamoja na upungufu wa mabweni na vitambulisho, siku chache baada ya serikali kuridhia madai ya wenzao wa Dodoma.

Mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), ambao ulisababisha vurugu na uharibifu kabla ya serikali kusalimu amri, ulifuatiwa na mgomo wa wanafunzi wa Chuo cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang'ombe (Duce) ambao walitulizwa kabla ya kuanza kugoma.

Jana wanafunzi wa Ardhi walianza kutekeleza uamuzi wao wa kugomea masomo baada ya Bunge la Wanafunzi kutoa baraka ya kutumia njia hiyo kuishinikiza serikali kutatua matatizo yao ambayo ni pamoja na kuondolewa kwa mkurugenzi wa shahada ya kwanza na mshauri wa wanafunzi kwa madai ya kuchelewesha kupeleka majina bodi ya mikopo na kufanya kazi za usajili badala ya kuwashauri wanafunzi.

Pamoja na kero hizo, wanafunzi hao pia wanataka kubadilishwa kwa vitambulisho, kuongezwa kwa mabweni, kumalizwa kwa tatizo la uhaba wa walimu na vifaa vya kujifunzia, upungufu wa vitabu na kuboreshwa kwa kantini za wanafunzi.
“Mazingira haya magumu yamesababisha baadhi ya wanafunzi wa kike kufanya matendo ya kikahaba na wanaume kufanya vutendo vya wizi ili kujipatia kipato,” alisema rais wa Serikali ya Wanafunzi (Aruso), Tegemeo Sambili.

Wanafunzi hao wanamtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda afike kuwatatulia kero zinazowakabili chuoni hapo na kwamba madai yao ya msingi ni pamoja na kero upungufu wa mabweni chuoni hapo inayowasababisha wengi wao kulala nje.
Akizungumzia kero hiyo, Sambili alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu yanayowashawishi kujiingiza katika matendo yasiyofaa.

Sambili alisema wanafunzi wamekuwa wakichelewa kupata mikopo kutokana na uongozi kuchelewa kupeleka majina yao Bodi ya Mikopo na hivyo kusababisha waishi maisha ya shida kutokana na fedha kuchelewa kuwafikia.

“Kutokana na hayo wanafunzi wamechoshwa na utendaji kazi wa Dk Liwa kama mkurugenzi kwa kuwa amekuwa akisababisha matatizo mengi; amekuwa akichelewesha kupeleka majina kwenda Bodi ya Mikopo kutoka kwenye ofisi yake na kusababisha wanafunzi kuchelewa kupata pesa kwa wakati,” alisema Sambili.

Naye spika wa bunge la wanafunzi, Jikora Emmanuel alisema kuwa kukosekana kwa vitambulisho vya wanafunzi ni tatizo jingine linalowasumbua kila wakati na kuwa mpaka sasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawana vitambulisho wakati wale wa mwaka wa pili wamepewa vikarakasi tu.

“Uongozi wa chuo uliahidi kutoa vitambulisho vyenye hadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu lakini hadi sasa hakuna lolote lililofanyika. Wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawana kabisa na hivi sasa wana wiki saba tangu walipojiunga na chuo,” alisema Emmanuel.

Awali wanafunzi walimtaka makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idrisa Mshoro kufika na kuzungumza lakini hawakufanikiwa na ndipo walipoamua kufunga mlango wa jengo la utawala.

Profesa Mshoro alizungumza na wanafunzi baada ya kufika kwa mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana na kuwatuliza wanafunzi hao baada ya kufanya naye mazungumzo.

“Naombeni niende ndani nizungumze na mkuu wenu ili nijue matatizo yenu na namna ya kuwasaidia,” alisema Rugimbana

No comments:

Post a Comment