KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, December 28, 2010

Wakili Aliyetuhumiwa Kumuua Mkewe Ashinda Rufaa


WAKILI Gabriel Mnyele aliyehukumiwa kifungo cha nje cha miezi 18 na
Mahakama Kuu Dar es Salaam baada ya kupatikana na hatia ya kumuua
mkewe bila kukusudia, ameshinda rufaa.
Mnyele alifutiwa adhabu hiyo mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Jaji Salum Massati, Mbarouk Mbarouk na Benard Luanda baada ya kutengua hukumu ya Mahakama Kuu juzi.

Mahakama ilifuta hukumu hiyo baada ya kuridhika na utetezi wa mawakili
wa mrufani huyo kuwa Mahakama Kuu ilikosea kumtia hatiani kwa kuwa
hukumu hiyo iliegemea ushahidi wa mazingira na upande wa mashtaka
ulishindwa kuthibitisha tuhuma dhidi yake.

Mnyele alihukumiwa Oktoba 19, mwaka jana na Jaji William Mandia wa mahakama Kuu kwa kosa la kumuua mkewe, Pamela Ngunyali kosa alilokuwa akituhumiwa na kukata rufaa kupitia kwa mawakili wake wanaomtetea,Mabere Marando na Richard Rweyongeza.

Moja ya kasoro zilizobainishwa na mawakili wa rufaa huyo ni kitendo
cha upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha mahakamani jalada la
matibabu na kushindwa kuthibitisha chanzo cha kifo cha marehemu, hoja
ambayo iliungwa mkono na Mahakama.

Mahakama ya Rufaa ilisema kitendo cha kutokuwepo kwa kumbukumbu za matibabu za marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kilisababisha kutokuwepo kwa kiungo cha ushahidi huo wa mazingira
katika kesi hiyo.

“Kwa hiyo tumeridhika kuwa ushahidi wa mazingira kwenye rekodi umeshindwa kukidhi matumizi ya aina hiyo ya ushahidi katika kuthibitisha kuwa ikiwa sababu ya kifo cha marehemu ilikuwa ni
majeraha ya kichwani na mrufani ndiye aliyesababisha majeraha hayo,”
ilisema Mahakama.

“Kwa sababu hizo hapo juu tunaikubali rufani na tunatengua hatia na
katika kutekeleza uwezo wetu wa kisheria, pia tunatengua adhabu
iliyotolewa katika Mahakama Kuu,” ilieleza hukumu ya majaji hao.

Awali, Mahakama ya Rufaa ilisema upande wa mashtaka ulipaswa kuwaita mahakamani mashahidi waliomtibu marehemu katika Hospitali ya Muhimbili, si tu kutoa maelezo ya matibabu, bali pia kuweka wazi
mashaka juu ya chanzo cha kifo cha marehemu.

Aidha, Mahakama hiyo ilisema kuwa hoja nyingine ni upande wa mashitaka
kushindwa kushughulikia kitendo cha Dk. Mwakyoma kufika mahakamani bila kuwa na jalada la kumbukumbu za matibabu ya marehemu, kitendo walichodai kuwa ni athari kubwa katika kutenda haki.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Mnyele alisema “nimefurahi sana kuwa haki imetendeka, nimeonekana sina hatia na jina langu sasa limesafishika na namshukuru Mungu kwa yote yaliyopita.

Jambo hili lilikuwa likinisumbua sana maana lilinizuia mambo mengi, lakini sasa nitaingia kwa nguvu katika kugombea ubunge wa Afrika Mashariki.”

Awali, ilidaiwa kuwa Mnyele alikuwa akikabiliwa na shitaka la kumuua
mkewe Pamela Ngunyali kwa kumpiga ofisini kwake katika jengo la Hugo
Kinondoni baada ya kugombana.

Ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Mnyele alimpiga mkewe huyo Novemba
10, 2003 na kumsababishia majeraha ambapo alikimbizwa katika Hospitali
ya Dar Group kabla ya kuhamishiwa Muhimbili ambako alifariki dunia
Novemba 20, mwaka huo.

Kwa mujibu wa taarifa za daktari, Pamela alifariki dunia kutokana na
majeraha ya kupigwa kichwani, lakini Mnyele katika utetezi wake alisema hakumpiga, bali alijikata kwenye mlango wa vioo ofisini kwake wakati alipotaka kumpiga teke

No comments:

Post a Comment