KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Mnigeria Awa Mbunge Wa Kwanza Mweusi Nchini Poland

John Abraham Godson akiapa kuwa mbunge
Mnigeria aliyelowea nchini Poland miaka 17 iliyopita na kuoa mwanamke wa Poland, amekuwa mbunge wa kwanza mweusi katika historia ya masuala ya siasa nchini Poland.
John Abraham Godson, alizaliwa katika jimbo la Abia nchini Nigeria na alikulia nchini humo kabla ya kuhamia nchini Poland.

Godsnon ambaye ni msomi mwenye shahada nyingi, amekuwa gumzo nchini Poland baada ya kuingia kwenye vitabu vya historia ya masuala ya siasa nchini humo kwakuwa mtu mweusi wa kwanza kuwa mtunga sheria wa bunge la nchi hiyo ambayo bado ina matatizo ya ubaguzi wa rangi.

Godson alishawahi kuonja joto la ubaguzi wa rangi nchini humo kwa kushushiwa kipigo mara mbili bila ya sababu za msingi.

Godson alihamia Poland mwanzoni mwa miaka ya 1990 na kuanzisha shule ya Kiingereza na pia kufanya kazi kama mchungaji wa kanisa la Kiprotestant.

Alimuoa mwanamke raia wa Poland na amefanikiwa kuzaa naye watoto wanne.

Alichaguliwa kuwa mbunge na chama cha Civic Platform Party, baada kiti cha ubunge wa jimbo lake kuwa wazi baada ya aliyekuwa mbunge kukiacha kiti hicho alipochaguliwa kuwa meya. Kabla ya kuwa mbunge alikuwa mjumbe wa baraza la halmashauri ya mji wa Lodz.

Kuhusiana na ubaguzi wa rangi nchini Poland, Godson alisema kuwa ubaguzi wa rangi nchini Poland umeanza kupungua katika miaka ya karibuni baada ya Poland kujiunga na Umoja wa Ulaya miaka sita iliyopita.

Akiongea na radio moja ya nchini humo, Godson alisema: "Mimi natoka Lodz (jimbo analoliwakilisha, nitaishi hapa, nitafia hapa na nataka nizikwe hapa".

No comments:

Post a Comment