KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 15, 2010

Mawakili watakiwa kuacha dhuluma


James Magai

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, amewataka mawakili kuacha dhuluma, tamaa ya kujikusanyia mapato na badala yake, watoe kipaumbe katika kuwahudumia wanyonge kwa kuzingatia kuwa kazi hiyo ni wito.

Jaji Ramadhani aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, alipokuwa aizungumza katika sherehe za kuwasajili mawakili wapya 337 wa kujitegemea.

Sherehe hizo zilifanyika katika Viwanja vya Karimjee.

Kiongozi huyo wa mahakama anayetarajiwa kustaafu rasmi Desemba 28 mwaka huu, alisema katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ambacho amekuwa madarakani, ameshuhudia dhuluma nyingi, zikiwemo zinazofanywa na mawakili.

“Mtindo huu katu ninyi mawakili wapya msiufuate. Nawasihi mfuate miiko ya kazi. Kipato kamwe msikipe kipaumbele. Mawazo yenu yote na nguvu zenu zielekezwe katika kuwatetea wanyonge. Uwakili kwa hakika siyo biashara bali ni wito,”alisema Jaji Ramadhani.

Aliwataka mawakili hao wafuate kile alichokiita kuwa ni kielezo alichowapa, kwa jinsi alivyojitoa na kuwasaili hata kwa muda wake wa ziada na hatimaye kuwathibitisha kwamba ni wanasheria wanaofaa.

“Ninyi wenyewe mmeona jinsi nilivyojitoa ili kuwasaili na kuwathibitisha kuwa mnafaa kusajiliwa kuwa mawakili. Nimefanya kazi hiyo Jumamosi na hata Jumapili,"alisema.


Mkongwe huyo wa sheria aliongeza kuwa "nimekaa ofisini mwangu wakati mwingine hata saa kumi na moja na hata saa kumi na moja na nusu jioni nikiwahudumia. Hii ni kwa sababu nimeona uchungu kuwaacha hadi mwezi Juni mwakani 2011.”

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, Felix Kibodya aliwataka mawakili hao watambue kuwa wao ni kioo cha jamii.

Aliwataka wawe waungwana katika kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi huku wakizingatuia kuwa Watanzanai wengi, hawana uwezo wa kulipia gharama za huduma za uwakili.

Kibodya pia aliwataka mawakili hao kuzingatia maadili ya kazi na kujifunza kutunza fedha za wateja wao, ili kuepuka kuitia doa fani yao.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema, katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Geoge Masaju, aliwataka mawakili hao kuishi kwa misingi ya kanuni za taaluma yao.

Alisema wao kama maofisa wa mahakama, kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha kuwa mwenendo wake na uendeshaji wa shughuli zake mahakamani, vinakidhi malengo ya haki na kudumisha uadili wa mfumo wa mahakama.

Edited by Ally Mkoreha

No comments:

Post a Comment