KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 30, 2010
Maaskofu wambana JK
VIONGOZI wa dini wamemuonya Rais Jakaya Kikwete kwamba matatizo mengi ya kiutawala anayoyapata yanatokana na usaliti wa wasaidizi wake wa karibu huku wakisisitiza serikali itende haki ili kuepusha vurugu.
Wakihutubia kwa nyakati tofauti juzi usiku katika mkesha na jana wakati wa ibada sikukuku ya Krismas, viongozi hao walionekana kukerwa na nchi kukosa dira pamoja na masuala mazito nchini kuendeshwa kwa kubahatisha.
Vilevile, wamehofia kutokuwepo kwa mikakati ya makusudi ya kuwanusuru wananchi na matatizo yanayowakabili.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite, Stephen Mang’ana alisema baadhi wa viongozi wa CCM na serikali wanamsaliti Rais Kikwete kwa kumpa taarifa za uongo na uchochezi ili wapate nafasi ya kuendelea kuwepo madarakani.
Kauli hiyo ya Mang’ana inakuja siku chache baada mtandao wa Wikileaks kuchapisha habari kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Dk Edward Hosea, kudaiwa kufichua siri za Rais Kikwete akisema hawezi kupambana na rushwa kwa vile amemzuia kuwafikisha mahakamani vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Akizungumza jana katika misa ya kitaifa ya Sikukuu ya Krismasi jijini Dar es Salaam, Mang'ana alisisitiza baadhi ya viongozi wa serikali sio waadilifu, hawana utashi wa Mungu wa kuongoza wananchi na kwamba wanachangia kuwepo migogoro.
Alisema viongozi wamekuwa wakitumia migogoro kujisafisha kwa wananchi jambo ambalo amesisitiza linahatarisha amani na utulivu nchini.
“Baadhi ya viongozi hawana utashi wa kuongoza, wapo kwa ajili ya kumsaliti Rais Kikwete na kusababisha kuwepo kwa migogoro kila sehemu, kuchochea vurugu na maandamano hasa katika baadhi ya maeneo,” alisema Mang’ana.
Kufuatia hali hiyo amewataka wananchi kuwa makini na viongozi hao, kwa kuwa hawana huruma na wapo kwa mslahi yao binafsi.
Alisema kitendo cha kutokuwa na washauri wazuri kumechangia baadhi ya wajanja kutumia nafasi hiyo kupandikiza chuki, jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.
Mang’ana, aliwakumbusha viongozi kuwa wanapaswa kuwa waadilifu ili waweze kufanya kazi zao kwa matakwa ya Mungu na si vinginevyo na kwamba waonyeshe uaminifu wao kwa kutenda mema.
Mwadhama Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebio Nzigilwa alisema hatua ya mtandao wa Wekileaks kuingia nchini na kutoa siri za serikali na viongozi wake ni fundisho kwa viongozi wabadhirifu.
“Mtandao huo ni sawa na chombo chochote cha habari kinachoweza kuandika habari za uchunguzi kuhusu serikali yoyote duniani hivyo basi, kama ina ushahidi wa kutosha kuhusu taarifa zao wanapaswa kuendelea,” alisema Askafu Nzigilwa.
Alisema kuwa, “Viongozi wabadhirifu wanapaswa kutambua kuwa wamewekwa madarakani na wananchi ili wawatumikie hivyo wanapaswa kuwa waaminifu wakati wote.”
Alisisitiza kauli yake kuwa ingawa hilo sio tamko la kanisa na wala kanisa halijakaa na kutoa tamko lolote kuhusu hatua ya mtandao, huo kuendelea kuwaumbua viongozi wa mataifa mbalimbali duniani, lakini hapendezwi na tabia ya viongozi wadanganyifu kwa wananachi wao.
Aliwataka wanadamu kuwa waaminifu mbele ya Mungu na hata mbele ya binadamu wenzao kwa sababu kukosa uaminifu ndiyo chanzo cha siri zao kuvuja.
Kuhusu hatua ya mtandao huo kumgusa Dk Hoseah alisema, “Viongozi waliotajwa na ambao hawajatajwa na mtandao huo wanapaswa kujirekebisha”.
Alisema hapendi kuona binadamu wakiumbuana wala mtu akiingilia kazi ya mwingine ama kufuatilia mambo binafsi ya mtu, lakini kama hiyo ndiyo itakuwa njia sahihi ya kuwarekebisha wanaofanya makosa, jamii haina budi kuukubali utaratibu huo.
“Twendeni tukasheherekee sikukuu ya kuzaliwa bwana wetu Yesu Kristo kwa amani na upendo na msijihusishe na vitendo vyovyote viovu wakati wa sikukuu na hata baada ya sikukuu,” alisisitiza Askofu Nzigilwa.
Kuhusu Katiba, alisema: “Katiba sio Biblia, ni maandishi yaliyoandikwa na wanadamu na kila mwanadamu anaweza kukifanyia mabadiliko kitu alichokiandaa.”
Alisema Biblia ndiyo kitabu pekee kilichoshushwa moja kwa moja kutoka mbinguni na ambacho mwanadamu hawezi kukifanyia mabadiliko na sio katiba ya nchi.
Alisema katiba ya nchi inaweza kubadilishwa muda wowote kulingana na mahitaji ya wananchi ambapo madai ya katiba mpya yameanza kupata baraka ya viongozi wa juu serikalini baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukusudia kumshauri Rais kuhusu suala hilo.
“Nisingependa kulizungumzia suala hilo kwa undani zaidi kwa sababu Waziri Mkuu ameshalizungumzia na ukizingatia kuwa Waziri Mkuu ni kiongozi mkubwa serikalini mimi sina cha kuongeza sana.”
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) Zakaria Kakobe alisema tathmini zilizofanywa baada ya uchaguzi mkuu hazikuwa za haki.
Kakobe alisema tathmini hizo zililenga kumjenga mgombea wa chama tawala ambaye anadai hakustahili kupewa haki hiyo.
“Makusudi ya kuja kwa Yesu Kristo ni kuleta amani iliyoambatana na haki, inapotokea katika nchi au jamii fulani haki ikakosekana, amani pia itapotea na kuleta machafuko,” alisema Kakobe
Akaongeza:“Chanzo cha machafuko ni inapofikia mtu amepewa haki isiyokuwa yake na yule anayestahili haki hiyo akanyimwa,”.
Kakobe alisema Tanzania inasifika kwa amani na utulivu, kutokana na waasisi wa nchi kutoa haki kwa wananchi na kwamba kwa sasa misingi hiyo haizingatiwi.
Alisema kila chama cha siasa kinatakiwa kupewa haki kama chama kingine na kuwa watu wanatakiwa kuondokana na fikra za kuwa na chama kimoja kinachoshika madaraka ndio chenye haki.
"Jamii inatakiwa kuondokana na fikra potofu za chama kimoja kushika hatama ya uongozi, huo ni ukale, na hiki ni kizazi kingine,” alisema Kakobe.
Hata hivyo, Kakobe aliwataka viongozi kuacha kuzungumzia udini badala yake wazungumzie haki na masuala yanayochochea maendeleo ya taifa.
Mkururugenzi wa Shirika la Familia la Farijika nchini Tanzania na Kenya, Padri Baptiste Mapunda alisema viongozi wa siasa ndio wanaochochea udini.
Padri Mapunda alisema viongozi wa siasia wamekuwa wakiibua hoja kwamba nchi ina udini ili waendelee kutawala.
Padri huyo aliyekuwa akizungumza kwa ukali huku akipigiwa makofi na mamia ya waumini alisema, “Nchi haina udini kama wanavyodai wanasiasa, wanatapatapa tu, walitakiwa watuulize sisi viongozi wa dini kama kweli nchi hii ina udini.
Alikwenda mbali na kusema viongozi wa siasa wanataka kuleta vita ya udini iliyokemewa vikali na serikali ya awamu ya kwanza ya hayati Mwalimu Julius Nyerere na akawataka Watanzania kuikataa dhambi hiyo.
Kuhusu katiba, alisema umefikia wakati kwa Watanzania wote kushirikishwa katika uundwaji wa katiba mpya na si kuziba kubadilisha vipengele.
“Napingana na kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu suala la katiba mpya, hapa hoja si kumshauri rais wala kuziba viraka, Katiba ni ya wananchi si ya rais, tunataka katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi,” alisema Padri Mapunda.
Alisema hivi sasa nchi inaelekea kubaya hadi kufikia hatua Jeshi la Polisi kuwapiga wabunge na wanafunzi wanaozungumza mambo kwa maslahi ya taifa na afafanisha matendo hayo na utumwa.
“Yesu alikuja duniani kukemea utumwa, sasa iweje mambo haya yatendeke Tanzania, umeme bei juu?, nchi ina wasomi wengi lakini wanashindwa kutumia elimu zao kuikomboa, hawa wasomi wamebaki na usomi wa darasani tu,” alisema Padri Mapunda.
Alifafanua kwamba wasomi wanatumia ujinga wa Watanzania kuwaburuza kutokana na ufinyu mdogo wa uelewa wa elimu ya uraia.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki, Mwashamu Kadinali Pengo, amewataka wenye uwezo kutokuwa na ubinafsi wa kujilimbikizia mali nyingi na badala yake wawasaidie wenye hali ngumu ya maisha.
“Najua kuna baadhi ya matajiri tena wanauwezo wa kifedha lakini wanakuwa wabinafsi,” alisema Askofu Pengo.
Alisema jamii inaamini kuwa, mtu akijilimbikizia mali ndio zitazidi kuongezeka siku hadi siku na kwamba hayo ni mawazo potofu na kutoweza kuwasaidia maskini ni kujitafutia hasara.
Alisema yeyote anayehubiri amani, lazima kwanza awe na amani moyoni mwake na suala la kuleta ama kulinda amani ni jukumu la kila mtu na haiwezi kuletwa na viongozi au mataifa makubwa kama ambavyo baadhi ya watu wanafikiria.
“Amani haiji kwa mabavu bali kwa paji la Mwenyenzi Mungu, amani haitegemei wenye mamlaka bali ni kila mmoja wetu bila kujali mali zetu, ilimradi tumtumikie bwana na kutenda mema.
“Siyo kama wakuu wa nchi ambao huketi chini kusaini mikataba ya amani, lakini kabla hata wino haujakauka, damu zimeshatapakaa mitaani kutokana na upotevu wa amani,” alisema Pengo
Askofu wa Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk Valentino Mokiwa aliunga mkono hatua zinazochukuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kwa kuwataka wananchi waliochukua viwanja vya wazi kuvirudisha.
Mokiwa alisema viwanja hivyo ni mali ya watoto na wananchi kwa ujumla na kwamba havikutengwa kwa ajili ya biashara na makazi.
Aliwataka wadau wa elimu na ardhi kuhakikisha viwanja hivyo hasa vya michezo vinarudishwa ili watoto wapate sehemu za kujifunza mambo mbalimbali yanayoweza kuwajenga katika maisha yao.
Paroko wa kanisa Katoliki parokia ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi Mugumu Serengeti, Padri Alois Magabe alisema vitendo vya uchakachuaji vinazaa dhuluma,uonevu,manyanyaso na mateso kwa watu wengi na ni matunda ya nguvu ya shetani aliyeteka nyoyo za watendaji.
Alisema uchakachuaji wa mambo yanayogusa jamii una madhara makubwa kwa jamii husika na wanaofanya hayo hawana roho ya Mungu ndani yao, kwa kuwa ni mateka wa ibilisi na kuzaliwa kwa Kristo kunatakiwa kuwabadilisha.
“Hata zamani uchakachuaji ulikuwepo, Eva alimchakachua Adamu kwa kutumiwa na shetani na matokeo yake dhambi iliingia duniani na mateso yakaanza na wanaofanya kwa sasa vitendo hivyo vinavyoleta mateso kwa jamii wanahitaji kuzaliwa upya na Kristo,” alisema Padre Magabe.
Akaongeza:“Mfalme wa amani amezaliwa mwenye uweza mabegani kwake anatakiwa kuwabadilisha wale wanaohusika na vitendo hivyo ili kuleta nafuu kwa
wananchi walio wengi,maana hakuna njia tofauti ya kujinasua zaidi ya kukubali kubadilisha maisha na tabia zao kwa njia ya Kristo.
“Vitendo vya uchakachuaji si vizuri kwa kuwa vinabadili haki na kuleta dhuluma ,uonevu,ukatili,na maisha magumu kwa watu. Si vya kunyamazia lazima tuwatake wahusika wazaliwe upya na Kristo mwenye uweza wa ajabu,” alisema bila kufafanua uchakachuaji upi.
Paroko Romuald Massawe wa Parokia ya Mwenyeheri Mtoni Kijichi, aliwataka waumini kutotumia nguvu katika kutafuta amani hali ambayo huleta machafuko na kulipelekea taifa katika hali mbaya.
Massawe alisema amani katika familia ni lazima idumishwe kwa kufanya mazungumzo pale inapotokea kutoelewana baina ya wanafamilia wenyewe.
Massawe alisema Watanzania wanatakiwa kukataa tamaa za kidunia kama kujilimbikizia mali na madaraka.
Kwa upande wa Kanisa la Angalikana Jimbo la Zanzibar limesema wakati umefika kwa viongozi wa serikali ya Zanzibar kuangalia mfumko wa bei za vyakula ambayo unaendele kuwaathiri wananchi wanaowaongoza.
Mchungaji Michael Hafidh katika mkesha wa ibada ya krismasi uliyofanyika katika kanisa la Mkunazini Mkoa wa Mjini Magharibi alisema, “Hatuhitaji kusikia maisha bora kutoka kwa viongozi wa serikali wakiwa mjukwaani ila ni
lazima wachukue hatua za makusudi na za lazima kuleta matumaini hayo kwa jamii.”
Askofu wa Kanisa la Katoliki Zanzibar, Augostino Shao aliwataka waumini kudumisha upendo, umoja na mshikamano.
Aligusia matumizi ya kondom na kusema kwamba sio kweli kama Papa Banedict karuhusu matumizi ya hayo na kuwataka waumini kujiepusha na vitendo vinavyopelekea kukumbwa na maambikizi ya virusi vya ukimwi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment