KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 2, 2010
Kampuni 100 bora kusakwa
Sadick Mtulya
KAMPUNI ya Mwananchi Communications Limited(MCL) kwa kushirikiana na kampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya KPGM, zitafanya utafiti unaolenga kupata bora 100 za ukubwa wa wastani.
Utafiti huo umelenga kujua jinsi kampuni za ukubwa wa wastani zinavyokua kwa haraka, kuonyesha ubora wa biashara pamoja na kutangaza mafanikio yaliyofikiwa katika ujasiriamali.
Kampuni hizo zitapatikana kwa kuangalia viashirio vya kifedha, ukuaji wa mapato, faida, marejesho kwa wabia pamoja na uzalishaji wa fedha taslimu katika utafiti huo utakaofanyika mwaka 2011.
Akizindua mpango huo jana jijini Dar es Salaam, mhariri mtendaji wa MCL, Theophil Makunga alisema pamoja na mambo mengine utafiti huo umelenga kuwezesha kampuni hizo za ukubwa wa wastani kujipima kwa kujilinganisha na kampuni nyingine pamoja na kuziinua na kuwaonyesha watunga sera mchango wao katika kukua kwa uchumi.
“Ni faraja kubwa kwa MCL kupitia gazeti la The Citizen kuasisi utafiti huu wenye lengo la kutambua kuwepo kwa wajasiriamali na umuhimu wao," alisema Makunga ambaye kampiuni yake ya MCL pia huchapisha magazeti ya inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumapili, Sunday Citizen na Mwanaspoti, .
“Pia mpango huo umelenga kuzisaidia kampuni zenye ukubwa wa wastani katika ukuaji wake kwa kuziunganisha na watoaji muhimu wa huduma ikiwa ni pamoja na kuwajengea ushirikiano na watoa huduma hao kwa kudhamini tafiti zao na kuanzisha jukwaa maalum kwa kampuni 100 bora.’
Utafiti huo wenye kauli mbiu ya “Soko moja, Nafasi Zaidi”, utaitimishwa Mei, 2011 kwa kila kampuni iliyoshika moja ya nafasi 100 za juu kupewa tuzo.
Makunga alisema kampuni yoyote inaweza kushiriki isipokuwa benki, kampuni inayotoa huduma ya bima za uhasibu/taasisi za ushauri wa kifedha na kampuni za kisheria na kwamba vigezo vya kushiriki ni vitatu.
Vigezo hivyo ni kampuni iwe na mtaji wa kati ya Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni, iwe na taarifa za fedha za miaka mitatu ambazo zimekaguliwa pamoja na ambayo haijasajiliwa kwenye Soko la Hisa.
Washiriki kwenye utafiti huo watatakiwa kuwasilisha taarifa za viashirio nane vya kifedha ambavyo ni kukua kwa mapato na kipato, marejesho ya hisa zisizo na riba ya kudumu na mwenendo wa fedha taslimu.
“Utafiti pia utakuwa ukitaka kuangalia tabia kama vile kujiamini kibiashara, sera za usimamizi wa vipaji, ushiriki katika shughuli za kijamii na nafasi ya ubunifu katika uendeshaji wao,’’ alisema Makunga.
Naye mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko alishauri utafiti huo usiwaache wakulima wadogo kutokana na kuwa na mchango katika kukuza uchumi wa nchi.
“Changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni masoko ya uhakika, pamoja na mitaji. Utafiti usiwaache wakulima wadogo,’’ alisema Ole Naiko
Mkurugenzi mtendaji wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Christine Kilindu alisema wanaunga mkono utafiti huo na kwamba utaongeza msukumo na kuweka mazingira bora ya biashara.
Utafiti huo, ni wa kwanza kufanywa nchini, lakinin ulishaendeshwa nchini Uganda mara mbili (2009 na 2010) na mara tatu nchini Kenya kuanzia mwaka 2008
Nchi ya Burundi na Rwanda nazo zitafanya utafiti huo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment