KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Halmashauri 133 zashindwa kulipa wafanyakazi


MWENYEKITI wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu) Mkoa wa Dar es Salaam, Gerald Msanga, ametaka serikali kuu kuwachukulia hatua wakurugenzi wa halmashauri 133 nchini, kwa kutumia fedha za zilizotolewa kuwalipa wafanyakazi nchini kinyume na makusudio.

Akizungumza kwenye mkutano wa mwaka na Wafanyakazi wa Talgwu Wilaya ya Temeke juzi, Msanga alisema fedha za bajeti za hamashauri ambazo hutolewa na serikali, zimeonekana kutumika tofauti na utaratibu unaotolewa.

Msanga alisema hatua ndio chanzo cha malalamiko ya kutolipwa madai mbalimbali ya wafanyakazi nchini.
Alisema ni halmashauri 16 pekee nchini ambazo zimelipa madai mbalimbali ya wafanyakazi, huku 133 zikishindwa kufanya wajibu wake na kuzitumia fedha hizo vibaya.

“Chanzo cha matatizo yote ya madai ya wafanyakazi nchini, ni halmshauri kwa kutokuwa makini na fedha za ruzuku ambazo serikali inatenga kwa matumizi mbalimbali, ikiwamo kuwalipa wafanyakazi,” alisema Msanga na kuongeza:
“Haiwezekani halmashauri 16 ziwalipe wafanyakazi wake wote na 133 zishindwe, hapa kuna tatizo.

Hivyo serikali ifuatilie hili kwa kuwabana wakurugenzi na watendaji wengine ndani ya halmashauri hizo wataje zilikokwenda.”

Msanga alisema kazi iliyofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka jana, kufanya uhakiki wa madai sugu ya wafanyakazi hao nchini yanayofikia Sh12.3 bilioni, ilikuwa nzuri lakini kuna matatizo kwani wengine hawajalipwa hata wale waliobahatika wamepunjwa.

“Tulikuwa tunadai serikali Sh29 bilioni wafanyakazi wote nchi nzima, serikali baada ya kuyapitia madai yetu imekubali kulipa Sh12 bilioni, lakini bado kuna tatizo kati ya serikali na halmashauri zake,” alisema Msanga.

Alisema serikali inatoa fedha kwa halmashauri mbalimbali nchini, lakini zinaonekana kutumika tofauti na kulipa wafanyakazi na kwamba, wakurugenzi wanatakiwa kuwajibishwa.

Madai hayo ni fedha za matibabu, likizo, ada za masomo, uhamisho na usumbufu, posho za safari, malimbikizo ya mshahara, gharama za mazishi na madai mengineyo

No comments:

Post a Comment