KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Polisi wadaiwa kushiriki wizi wa makontena


Mwandishi Wetu
BAADHI ya askari polisi wanadaiwa kushirikiana na mtandao wa ujambazi unaoendeshwa kwa kushirikiana na genge la wahalifu kupora mali na kunyanyasa wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi.

Wahalifu hao wamekuwa wakiteka magari ya mizigo inayosafirishwa kwenda mikoa au nje ya nchi na malori hayo kupelekwa njia tofauti ambako mizigo hupakuliwa bila ya idhini ya mwenye mali.

Habari zinasema kuwa mzigo ambao ulikusudiwa kupelekwa Burundi huingiliwa njiani na kuelekezwa barabara iendayo Arusha na njiani polisi walio kwenye mtandao huo hufanya mawasiliano na wenzao ili kulinda wasiikamate endapo watabaini kuwa nyaraka za mizigo hiyo zinaonyesha njia tofauti.

Habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kwamba mtandao huo umejikita katika barabara itokayo Dar es Salaam kwenda Arusha na ile ielekeayo nchi jirani za Burundi na Rwanda.

Polisi hao wamekuwa wakishirikishwa kwenye mtandao huo kwa kufanya mawasiliano ili kuhakikisha usalama wa majambazi hao baada ya tukio la kupora.

Habari hizo, ambazo zimethibitishwa na baadhi ya makamamnda wa polisi wa mikoa, zinadai kuwa katika kuhakikisha wahalifu hao wanakuwa salama baada ya kupora, askari wa Jeshi la Polisi wanadaiwa kuwaweka ndani watu wanaotoa taarifa za matukio ya uporaji.

Mtandao huo umeelezwa kudiriki hata kuwatesa watu wanaotoa taarifa za kuporwa kwa mali zao na hata kuwatishia maisha ili kuwafunga mdomo.

"Ni kweli kuna wizi wa namna hiyo," alisema kamanda wa polisi wa mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile lakini akaongeza kuwa mtu aliyelalamika ambaye suala lake liko kituo cha Msimbazi ndiye anayetuhumiwa kwa ujambazi.
"Mimi mwenyewe ndiye niliamrisha akamatwe na tutamfikisha mahakamani kujibu mashtaka.''

Katika tukio la hivi karibuni, polisi wa kituo cha Msimbazi wanadaiwa kumweka ndani mtendaji na ofisa wa kampuni moja ya kusafirisha mizigo ya jijini Dar es Salaam ambao walikwenda kituoni hapo kutoa taarifa za wizi wa mizigo yenye thamani ya Sh90 milioni iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea mkoani Mbeya.

Mizigo hiyo iliibwa na kusafirishwa kuelekea mkoani Arusha.

Kama hiyo haitoshi, polisi hao waliwakamata na kuwasweka lupango maofisa wengine wa kampuni hiyo waliokuwa na maelezo ya namna mali zao zilivyoporwa.

Waporaji hao walikamatwa na polisi pamoja na gari walilotumia kutorosha mali hizo, lakini baadaye waliachiwa katika mazingira yaliyoelezwa kuwa ni tata. Habari zinasema kuwa hata mtu aliyekutwa akiwa ameficha nyumbani kwake sehemu ya mali zilizoporwa, aliachiwa bila kufikishwa polisi kutoa maelezo.

Hata hivyo, gari lililosafirisha mzigo huo (namba tunazo) ambalo baadaye lilikamatwa mjini Moshi likiwa limebeba sehemu ya mzigo huo na kupelekwa kituo cha Msimbazi ambako jalada la wizi huo lilifunguliwa. Gari hilo liliruhusiwa kuondoka kituoni Jumanne wiki hii, huku sehemu ya mzigo uliokamatwa ambao ungetumika kama kidhibiti, ukiteremshwa kutoka gari hilo.

Inadaiwa kuwa kabla ya gari hilo kuachiwa, wamiliki wake ambao wana asili ya Kisomali walionekana wakifanya vikao vya siri pamoja na mawasiliano ya simu na polisi ambao wanaonekana kuwa kwenye mtandao huo na ambao vituo vyao vya kazi ni Dar es Salaam, Moshi na Arusha.

Wakati wahalifu hao wakiachiwa huru, inaelezwa kwamba walalamikaji waliendelea kusumbuliwa kwa kuwekwa rumande na katika vituo vya polisi tofauti mkoni Arusha, Moshi na Dar es Salaam na kuambiwa kuwa wao ndio wahalifu.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wafanyabiashara hao Geogre Mateso anayemiliki kampuni ya Mateso Group & Company Limited alieleza kushangazwa kuona polisi wakiwasumbua watu wema wanaotoa taarifa za uhalifu.
"Badala ya watu wema kuona polisi ni mahali salama pa kukimbilia, kwetu hali ti tofauti," alisema.

"Sisi tuliotoa taarifa za uhalifu wa mali tulizokuwa tukisafirisha, ndio tuliofanyiwa unyanyasaji na kuwekwa rumande. Cha ajabu ni polisi hao kuwachia wamiliki wa magari yaliyotumika katika uhalifu pamoja na madereva waliohusika."

Aliongeza kusema: “Tunakimbilia polisi kutafuta msaada wa kupata haki zetu, lakini inakuwa kinyume. Tunaotafuta haki tunadidimizwa; tunaodai ndiyo tunakamatwa na kuwekwa ndani; pesa tunatolewa na polisi Msimbazi.

"Sipo peke yangu najua yapo makampuni mengine yenye shida kama yangu hapo Polisi Msimbazi.”

Alisema mkasa huo ulimkumba Oktoba 27, mwaka huu wakati kampuni yake ikisafirisha mzigo kwenda Mbeya.
Alisema kuwa walipofuatilia walibaini kuwa mzigo huo haukupelekwa Mbeya na badala yake ulipelekwa mkoani Arusha.

Alisema kuwa alitoa taarifa polisi Novemba tatu mwaka huu na kupewa RB namba MS/RB/12331/2010 pamoja na barua kuwawezesha kufuatilia suala hilo mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.

Baada ya kufuatilia walibaini kuwa gari hilo lilipita na kupima uzito katika mizani ya Chalinze Oktoba 28.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, walifuatilia mizigo hiyo hadi Moshi mkoani Kilimanjaro na kupewa askari waliokwenda nao hadi Arusha.

Alisema walifanikiwa kukamata sehemu ya mzigo huo tani 10 kwa mkazi mmoja wa Himo baada ya kulikamata gari lililobeba mzigo huo Namanga ambako ni mpakani mwa Tanzania na Kenya.

Hata hivyo, alisema baada ya kupata taarifa ya gari hilo kuonekana eneo la Namanga, waliwekwa rumande mkoani humo kwa siku nne kuanzia Novemba 7 hadi Novemba 10 na kubadilishiwa 'kibao' wakituhumiwa kwa wizi.
"Tulitaka kufuatilia tukiwa pamoja na askari na wakala wa mmiliki wa gari, lakini sisi tukazuiwa kwenda; wakaenda polisi na huyo wakala, badala yake sisi tukawekwa ndani siku nne," alilalamika mmiliki huyo wa kampuni ya usafirishaji.

Wakati walalamikaji wakiwa rumande, inadaiwa wahalifu hawakukamatwa licha ya kukutwa na mali hizo za wizi jambo ambalo linaashiria kwamba kulikuwa na mchezo mchafu kati ya polisi na watuhumiwa hao wa uhalifu.

Watu hao pia waliwekwa rumande walipokwenda kituo cha Msimbazi, Dar es Salaam ambako pia inadaiwa kuna kesi nyingine tano za watu wanaolalamikia mizigo yao kuibwa katika mazingira hayo yanayoelezwa kuwa ya utata.

Mwananchi imedokezwa kuwa katika tukio moja la hivi karibuni, mmoja wa polisi anayeshiriki kwenye mtandao huoalimtisha mtu aliyekuwa anafuatilia mizigo yake iliyoporwa na wahalifu hao na kumkejeli kuwa "haki mbinguni pekee".

“Kama hamjui duniani hakuna haki, mtajua leo! Haki ipo mbinguni tu,” mmoja wa wapashaji wetu alimnukuu polisi huyo ambaye ni mmoja wa vigogo wa jeshi hilo wanaojihusisha na mtandao huo katika njia ya Dar es Salaam na Arusha.

Kituo cha polisi cha Msimbazi jijini Dar es salaam kimetajwa kuwa kina maofisa wengi wanaojihusisha na mtandao huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, inapotokea askari polisi aliye nje ya mtandao huo amekamata mali au miongoni mwa wanaojihusisha na genge la uhalifu, juhudi kubwa hufanyika ili kesi isiende mahakamani na baadaye watuhumiwa huachiwa pamoja na gari walizotumia huku walalamikaji wakinyanyaswa na kuwekwa rumande hadi uhalifu unapokamilika.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba matukio ya namna hiyo yanawakumba wafanyabiashara wengine, wakiwepo wale wanaosafirisha mafuta kwenda nchi jirani.

“Malalamikio haya hayakufanyika kwa mfanyabiashara huyo pekee. Wapo mengi na unyanyasaji huo upo hasa kitengo cha upelelezi. Kila ukienda kuripoti tukio la uhalifu, wewe ndio utawekwa ndani bila maelezo. Kesho tena atawekwa mfanyakazi wako lakini kutoka lazima uwape fedha," alieleza mpashaji wetu.

“Kibaya zaidi ni kwamba mtu akiibiwa anawekwa ndani, lakini sehemu ya watuhumiwa wa wizi ambao wanamiliki gari lililobeba mzigo wanaachiwa huru.”

Mtandao huo wa uhalifu unadaiwa pia una mbinu nyingine ya wizi ya kujipatia fedha kwa njia haramu ya kuhakikisha kila msafirishaji anatoa fedha taslimu kila mali zao zinapopita kwenye vituo vyao.

Inadaiwa kuwa msafirishaji mmoja anayetoa mali yake kwenda Arusha au Mbeya hulazimika kutenga kati ya Sh 300,000 hadi 600,000 kuwapa wanamtandao hao ili kuepuka kunyanyaswa.

Habari zinadai kuwa mtandao huo wa kihalifu ndani ya Jeshi la Polisi una ushirikiano na makundi mengine ya kihalifu kwenye nchi jirani za Burundi na Rwanda.

Wahalifu hao wa nchi jirani inadaiwa kuwa wana silaha kali za kivita na hutekeleza uhalifu huo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo ya kanda ya Ziwa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alikiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini akasema anachojua katika kituo cha polisi Msimbazi lipo tukio moja la aina hiyo akitaja mhusika kuwa ni Mateso na kwamba ndiye anayehusika na matukio ya wizi.

"Sina taarifa ya matukio mengine ya wizi wa mizigo, kama yapo watu hao waje kuniona moja kwa moja. Lakini ninachojua ni kukamatwa kwa Mateso ambaye anatuhumiwa kwa wizi na ndiye anayehusika na uibaji wa mizingo,'' alisema Shilogile.

Kamanda Shilogile aliongeza kusema: ''Mimi mwenyewe ndiye niliamrisha akamatwe na tutamfikisha mahakamani kujibu mashtaka.''

Ingawa kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha hakupatikana kuzungumzia suala hilo jana, kamanda wa Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Lucas Ngh'oboko alisema hana taarifa za kuwepo kwa mtandao huo.

Hata hivyo alisema iwapo kuna wafanyabiashara waliopatwa na mkasa huo waende wakamuone ili ashughulikie suala lao.

"Sina taarifa ya hali hiyo, lakini kama wapo wasafirishaji waliofanyiwa hivyo na askari wangu, waje wanione nitalishughulikia," alisema.

Kama polisi wangu wanahusika na mtandao huo ikithibitika nitachukua hatua," alisema Kamanda Ngh'oboko.
Hata hivyo, alisema kuwa iwapo askari wake waliwaachia watuhumiwa bila kuwakamata huo ni uzembe ambao hautavumilika na akasisitiza kwamba apelekewe taarifa sahihi ili hatua zichukuliwe.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Advera Senso alisema: "Nitalichunguza suala hilo, lakini ni vyema anayetoa taarifa hizo kwako akatusaidia kujua zaidi namna polisi wanavyohusika na wizi huo."

No comments:

Post a Comment