KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Nyota wa Sinema Amuua Mama Yake Akidai ni Shetani


Nyota wa filamu wa Marekani amemuua mama yake kwa kumkata vipande vipande kwa kutumia jambia akidai kuwa alitumwa na mungu amuue shetani aliyekuwa ndani ya mwili wa mama yake.
Michael Brea mwenye umri wa miaka 31, nyota wa filamu ya "Step Up 3D" na tamthilia maarufu ya "Ugly Betty" ametupwa rumande akisubiria hukumu yake kwa kumuua mama yake kwa jambia.

"Sikumuua yeye, nimemuua shetani aliyekuwa ndani ya mwili wake", alisema Brea alipokuwa akiongea na gazeti la New York Daily News akiwa kwenye wadi ya hospitali ya jela ambako aliwekwa tangu alipotiwa mbaroni kwa kosa la mauaji.

"Niliendelea kumkatakata vipande vipande na hakuna mtu aliyeweza kunizuia. Nilikuwa nikifanya kazi ya mungu", aliendelea kusema Brea.

Kwenye majira ya saa saba na nusu usiku siku ya jumanne majirani walisikia kelele Brea akimwambia mama yake "Tubia tubia" huku akimsomea mistari ya biblia.

Majirani walisema kuwa Brea alikuwa akimkimbiza mama yake nyumba nzima huku akimlazimisha atubie.

Majirani waliita polisi ambao walipofika walikuta tayari Brea ameishamchinja mama yake.

Maiti ya mama yake, Yanick Brea, 55, ilikutwa bafuni ndani ya nyumba yake iliyopo Brooklyn, taarifa ya polisi ilisema.

Brea, alikutwa na polisi akiwa amekaa chumbani huku ameshikilia jambia lenye urefu wa futi tatu.

Ndugu wa marehemu wametoa taarifa ya kuonyesha kumtetea Brea ambaye wamesema alikuwa ni mwanaume mpole, mwenye huruma na mwenye mapenzi kwa mama yake lakini alikuwa akihitaji msaada kwa matatizo yaliyokuwa yakimkabili.

"Familia yake na marafiki zake wanajua fika kuwa Michael hakuwa akijitambua wakati alipokuwa akimuua mama yake", ilisema taarifa ya familia ya Brea

No comments:

Post a Comment