KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Mashangingi ya mawaziri yazua utata



Sadick Mtulya

WAKATI mawaziri na manaibu wawaziri wakikabidhiwa magari mapya, baada ya kuapishwa Jumamosi iliyopita, serikali imeibuka na kusema sio mapya ni ya zamani.
Kauli hiyo inaibua utata kutokana na kuwa baada ya kuapishwa viwanja vya Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, kila waziri alikabidhiwa dereva mpya na gari jipya aina ya Toyota GX V8,
badala ya gari aina ya Toyota VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na mawaziri waliopita.

Ununuzi wa Toyota GX V8 mpya, unashiria serikali bado haijawa tayari kuunga mkono msimamo wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye amekuwa akisikika akitaka kusitishwa ununuzi wa magari ya kifahari ili kupunguza matumizi ndani ya serikali.

Toyota GX V8 moja huuzwa kati ya Sh210 milioni hadi Sh240 milioni, hukuToyota VX V8 moja inauzwa sio chini ya Sh180 milioni.

Akizungumza na Mwananchi jana, Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, alisema magari hayo sio mapya na kwamba, yaliyotumiwa na mawaziri waliopita.
Rais Jakaya Kikwete ameigawanya iliyokuwa Wizara ya Miundombinu na kuwa wizara mbili; Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi.

“Yale magari sio mapya, yalikuwepo. Kwanza uliyaona au unasema tu, hamjayachunguza vizuri jamani, fanyeni uchunguzi,’’ alisema Chambo na kukata simu.
Mawaziri wote na baadhi ya manaibu walikabidhiwa magari hayo (GX V8), huku manaibu wengine wakikabidhiwa VX V8.
Sababu ya baadhi ya manaibu mawaziri kukabidhiwa VX V8 badala ya GX V8, ni kutokana na kutokamilishwa kwa taratibu za kutokamilika.

Mmoja wa manaibu mawaziri (jina tunalo), alikabidhiwa VX V8 iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifungo na Uvuvi, John Magufuli, ambaye sasa ni Waziri wa Ujenzi.
Gazeti moja la kila siku (si Mwananchi) limeeleza kuwa ununuzi wa magari hayo, umegharimu serikali Sh9.3 bilioni na kwamba, takwimu za iliyokuwa Wizara ya Miundombinu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2005/06 magari makubwa ya kifahari yapatayo 6,000 yalikuwa yamenunuliwa na serikali kwa gharama inayokadiriwa kufikia Sh160 bilioni.

Miongoni mwa magari hayo ni Toyota Land Cruiser (VX/ GX V8, Prado) yapatayo 1,655, Nissan Patrol na Land Cruiser 885, Mitsubishi Pajero 400 na mengineyo.
Tangu kipindi cha serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, kumekuwepo na mjadala kuhusu matumizi makubwa ya serikali hasa katika ununuzi wa magari ya kifahari kutokana na kuendeshwa kwa gharama kubwa.
Wadau wengi wanataka viongozi watumie magari ya kawaida kama ilivyo kwa nchi ya Kenya na Rwanda

No comments:

Post a Comment