KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Maalim Seif 'aiteka' Pemba



Salma Said, Zanzibar

WANANCHI mbali mbali wa Kisiwani Pemba, wamejitokeza kwa wingi kumlaki Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwa mara ya kwanza amefanya ziara yake kisiwani humo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mapema mwezi huu.

Uteuzi huo ulifanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Kuwasili kwa Maalim Seif katika kisiwa hicho alichozaliwa na ambayo ni sehemu ya Zanzibar, kuliwavutia mamia ya wananchi ambao walijitokeza kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Karume.

Wananchi hao walikuwa wamejipanga barabarani kama ishara ya kumuunga mkono kiongozi huyo ambaye sasa yuko katika serikali ya umoja wa kitaifa.

Pamoja na wananchi, pia kulikuwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wa kisiasa waliomlaki Maalim Seif ambaye baadaye, alipanda gari lake katika viwanja vya Tibirinzi ambako alifanya mkutano wa hadhara.

Katika viwanja hivyo, ngoma mbali mbali na burudani za kiasili , zilitawala kuashiria furaha ya wananchi wa Pemba kwa Maalim Seif.

Katibu wa Vijana wa Chama cha CUF, Khalifa Mohammed alisoma risala iliyowahimiza wananchi wote wa Unguja na Pemba, kuungana na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuleta maendeleo nchini.

Katika uwanja wa ndege, baadhi ya wananchi walisema hawaamini kwamba Maalim Seif angepokelewa na viongozi wa serikali huku akiongozwa na magari ya polisi, ili kuimarisha usalama wake.


"Nimekuja si kumuona Maalim Seif , lakini kujionea mwenyewe kama kweli anaongozwa na vimulimuli, ni kweli anafuatwa na walinzi, nilitaka nijionee mwenyewe," alisema Salim Said Kombo.

Idadi kubwa ya watu waliojitokeza kumpokea Makamu wa Kwanza wa Rais, walikuwa wamevalia mavazi yenye rangi zinazoitambulisha CUF na wengine walikuwa wamevaa fulana na kanga za CCM, kama ilivyokuwa juzi katika Uwanja wa Kibanda Maiti, mjini Unguja.

Akizungumza na wananchi, Maalim Seif aliwashukuru kwa kufanikisha uchaguzi mkuu kwa salama na kwamba kwamba uhusiano wake na viongozi wenzake wa serikali ni nzuri.

Alisema chini ya serikali ya umoja kitaifa, watafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Rais wake na pamoja na Makamu wa Pili wa Rais.

Alisema kwa msingi huo, wananchi wa Zanzibar, lazima watarajie maendeleo makubwa yatakayotokana na ushirikiano huo katika kutekeleza majukumu ya serikali.


Maalim Seif alisema yeye, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd watafanya kazi pamoja na kamwe hawatatoa nafasi kwa waovu, kuwavuruga.

Aliwahakikishia wananchi kuwa umoja na ushirikiano wao katika serikali, ndio utakaoleta mabadiliko ya haraka katika kuiendeleza Zanzibar .


Makamu wa Kwanza wa Rais, alisema katu hawatakubali kuwarejesha Wazanzibari katika siasa za chuki na uhasama na kwamba sasa ni wakati wa wananchi bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuiunga mkono serikali yao.

"Nakuhakikishieni mimi na rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd , ni kitu kimoja tumeshikamana sana na katu hatugawanyiki, Inshallah hatutoi nafasi kwa kidudu mtu kutugawa," alisisitiza.

Katika mkutano huo, Maalim Seif pia aliwatambulisha baadhi ya mawaziri walioteuliwa na Rais Dk Shein wakiwemo wale wa chama cha CUF na kuwataka wananchi wawaunge mkono na kuwapa ushirikiano mkubwa.

Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa kampeni za kistaarabu bila ya kuingiza matusi, chuki na jazba, zimesaidia kwa kiasi kikubwa,kupunguza matatizo yaliyokuwa yamezoeleka katika siasa za Zanzibar.

“Faida ya kampeni za kistaarabu tumeziona na leo hii tunakaa pamoja na kushauriana laiti tungefanya kampeni za kutukanana na kufanyiana chuki basi tungechukua zaidi ya miezi mitatu mimi na Dk Shein tungegombana," alisema.

Alisema urithi nzuri wa kuwepo kwa amani na utulivu ulioachwa na rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, unahitaji kuendelezwa na kila Mzanzibari, ili kuiletea nchi maendeleo na matumaini makubwa.

Pia alisema chini ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa, Zanzibar ni nchi isiyokuwa na Serikali ya Mapinduzi kama ilivyokuwa awali.


"Serikali ya sasa ina Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais na tunafanya kazi kwa maslahi ya wananchi wote wa Zanzibar,” alisema Maalim Seif.

Kiongozi huyo pia aliahidi kusimamia nidhamu na uadilifu wa viongozi wa serikali ili matarajio ya wananchi yafikiwe .


Wakizungumza katika mkutano huo wakati wa kujitambulisha mawaziri wanane na manaibu wawili walioteuliwa kutoka chama cha CUF waliahidi kuwatumikia wananchi wote wa Zanzibar bila ya ubaguzi

No comments:

Post a Comment