KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Fred Mpendazoe akamatwa


Sadick Mtulya
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea kwa tiketi ya Chadema, Fred Mpendazoe janaalipatwa na msukosuko wakati alipokamatwa na askari wa Jeshi la Polisi ambao walidai kuwa alikuwa anamiliki na kutumia gari la wizi, tukio ambalo amelielezea kuwa lilipangwa kwa lengo la kumchafua.

Mpendazoe, ambaye alishindwa kwenye uchaguzi huo wa ubunge kwa njia ambayo ameielezea kuwa ilijaa ukiukwaji wa sheria, alihojiwa na polisi kwenye kituo cha Buguruni kwa takriban saa mbili kabla ya kuachiwa bila ya masharti.

Mpendazoe, mmoja wa wabunge waliokuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya ufisadi, alikamatwa jana majira ya saa 3:30 asubuhi eneo la Uwanja Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na diwani wa Chadema wa Kata ya Segerea, Azuri Mwamboji pamoja na Buhari Mgonyezi ambaye aligombea udiwani wa Kata ya Kinyerezi.
Hata hivyo, Mpendazoe, ambaye alihama CCM mapema mwaka huu wakati akiwa mbunge wa Jimbo la Kishapu na kujiunga katika Chama cha Jamii (CCJ) na baadaye Chadema, aliachiwa majira ya saa 5:44 asubuhi na maafisa upelelezi wakamueleza kuwa wataendelea na uchunguzi.

"Kwa kuwa namba zako za simu umetuachia, wewe nenda. Sisi tutatimiza wajibu wetu wa kuendelea na uchunguzi. Hatua tutakayofikia tutakufahamisha,'' alisema afisa upelelezi mmoja.
Mpendazoe amefungua kesi Mahakama Kuu kupinga matokeo ya ushindi wa Dk Makongoro Mahanga kwenye Jimbo la Segerea, baada ya zoezi la kuhesabu kura kuingiwa na dosari kubwa zilizocheleweshwa kutangazwa kwa matokeo.
Hata hivyo, Dk Makongoro ameshateuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.
Mpendazoe anatuhumiwa kumiliki na kutumia gari la wizi aina ya Toyota Corona, lenye rangi nyeupe ambalo inadaiwa liliripotiwa kuibwa tangu Juni mosi, 2010.
Lakini mbunge huyo wa zamani wa Kishapu aliiambia Mwananchi jana kuwa tuhuma hizo zimelenga kumchafua na kwamba ni hujuma.

"Askari walinikamata kwa nguvu kubwa, hadi kufikia hatua ya kutishia kutumia silaha endapo ningeendelea na msimamo wangu wa kutaka kujieleza... sisi ni raia na katika mazingira haya inabidi tusaidiwe,'' alisema Mpendazoe ambaye aliruhusiwa kuondoka na gari hilo.
Alifafanua kuwa tukio hilo lilipangwa kwa makusudi na kusisitiza kuwa gari hilo ni lake na amekuwa akilimiliki tangu mwaka 2007.

"Hadi sasa polisi hawajaniambia ni mtu gani aliyefungua mashtaka haya (ya kudai kuibiwa gari hilo). Hii ni hujuma kutoka kwa watu ambao hawanitakii mema pamoja na dola kuendelea kunikandamiza. Gari nimelitumia katika kipindi chote cha kampeni zilizopita za uchaguzi mkuu,'' alisema.

"Jana (juzi) tu, nilikuwa nalo kituo cha polisi cha Sitakishari, Ukonga nilipokuwa nimekwenda kuomba kibali cha kufanya mkutano wa harambee ili kuwaomba wananchi kunichangia fedha kwa ajili ya kuendeshea kesi niliyofungua kupinga matokeo yaliyompa ushindi Dk Makongoro.''
Hata hivyo, Mpendazoe alisema kuwa polisi walimnyima kibali hicho na kulalama kuwa eneo alilokuwa amekusudia kufanya mkutano ndilo aliloruhisiwa Dk Mahanga wiki iliyopita kufanya mkutano wa kuwashukuru wakazi wa Segerea kwa kumchagua.

Mpendazoe pia alidai kuwa wiki iliyopita alitumia gari hilo kwenda kituo kikuu cha kati cha polisi kuomba kibali cha kufanya mkutano wa hadhara.
"Ajabu nyingine gari hili hili, wiki iliyopita nilikuwa nalo... mbona hawakunikamata,'' alihoji Mpendazoe.
Alikwenda mbali na kusema: " Kulingana na mazingira haya, hisia zangu ni kwamba hizi ni hujuma na demokrasia inaaza kukandamizwa.''

Kamanda wa Polisi Ilala, Faustine Shilogile hakutaka kuzunghumzia suala hilo kwa maelezo kuwa hakuwa ofisini.
"Nitafute baadaye; kwa sasa sina taarifa kamili na muda huu ( saa 6:30 mchana) nipo njiani natoka uwanja wa ndege.... naenda hapo kituoni,'' alisema.
Alipopigiwa simu baadaye, hakupokea

No comments:

Post a Comment