KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, October 28, 2010

Waziri wa Mambo ya Nje Kenya ajiuzulu



Waandishi wa Mwananchi, Nairobi

VIONGOZI wa juu wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini Kenya wamejiuzulu kukwepa shinikizo la Bunge la kutaka waachie ngazi kuruhusu uchunguzi dhidi ya kashfa za ubadhirifu na matumizi mabaya ya mali ya umma zinazowakabili. Wakuu hao, Moses Wetangula, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, na katibu mkuu wake, Thuita Mwangi walijiuzulu jana baada ya kuibuka kashfa za ubadhirifu katika mikataba mitano ya ununuzi wa majengo matano ya balozi za nchi hiyo kwenye nchi tofauti.

Viongozi hao wamejiuzulu muda mfupi baada ya Rais Mwai Kibaki kutangaza kwamba serikali yake haitakuwa na mzaha kwa kiongozi yeyote atakayetuhumiwa kwa rushwa na ufisadi. Wawili hao wamejiuzulu ikiwa ni wiki moja baada ya Rais Kibaki kutangaza kumsimamisha kazi Waziri wa Elimu ya Juu, William Ruto kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili za ubadhirifu baada ya mahakama kutoa uamuzi kwamba anatakiwa kujibu tuhuma hizo mahakamani. Uamuzi wa kujiuzulu kwa Wetangula, ambaye hata hivyo amesisitiza kwamba hana hatia, pamoja na katibu huyo ulifikiwa baada ya majadiliano baina yao na Rais Kibaki kwenye ofisi zilizo kwenye Jengo la Harambee.

Mwangi alianza kwuasilisha barua yake akifuatiwa na Wetangula. Kwa mujibu wa ripoti ya kamati malum ya Bunge, serikali ya Kenya imepoteza dola 14 milioni za Kimarekani katika mpango wa ununuzi wa nyumba kwa ajili ya ofizi za ubalozi wake nchini Japan, huku Wizara hiyo ikituhumiwa kwa ubadhirifu katika mikataba kadhaa ya aina hiyo iliyofanyika nchini Misri, Nigeria, Pakistan na Ubelgiji. Katika tuhuma hizo, Wizara ya Mambo ya Nje inadaiwa kukataa ardhi ya bure kutoka kwa serikali ya Japan katikati mwa jiji la Tokyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya za ubalozi na kuamua kwenda kununua jengo mbali na eneo hilo, tofauti na ushauri uliotolewa awali na wakala mshauri wa serikali. Wakuu hao walitangaza uamuzi wao wa kujiuzulu kabla ya Bunge kukamilisha mjadala wa taarifa ya kamati hiyo ya Ulinzi na Uhusiano wa Kimataifa.

Katika mjadala wa Bunge uliokuwa ukiendelea wakati wakuu hao wakitangaza kujiuzulu, lawama zilikuwa zikielekezwa kwa Wetangula ambaye juzi alielekeza lawama kwa maofisa wa wizara hiyo kwa kutokuwa makini katika suala hilo. Akitangaza uamuzi wake mbele ya waandishi wa habari waliokusanyika kwenye ofisi yake saa 3:00 baada ya kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais Kibaki, Wetangula alisema anamini kuwa yeye ni mtu safi asiye na hatia. "Nataka kuwaambia Wakenya kuwa dhamiri yangu iko wazi kwa uamuzi wangu mchana huu. Kwa hatua hii ya uwajibikaji wangu kama Waziri wa Mambo ya Nje ni kutoa nafasi kwa wale wanaonituhumu kufanya uchunguzi,” alisema. Wetangula amekuwa akijadiliwa sana katika katika kipindi cha wiki nne cha uchunguzi wa kamati hiyo ambayo inamalizia kukamilisha ripoti yake

No comments:

Post a Comment