KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, October 11, 2010

UN yaonesha wasiwasi Sudan
wananchi wa Sudan Kusini


Ujumbe wa Umoja wa Mataifa umemaliza ziara yake nchini Sudan kwa kutoa wito kwa nchi hiyo kuhakikisha kura ya maoni ya uhuru wa Sudan Kusini inafanyika katika wakati uliopangwa.


Wajumbe hao wa Umoja wa Mataifa wamesema ratiba ya kura hiyo ya maoni itakayofanyika mwezi Januari iko karibu mno, lakini "inawezekana" wamesema.

Kura hiyo ya maoni ni matokeo ya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 na kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Kaskazini na Kusini vilivyodumu kwa miaka 21.

Ghasia

Umoja wa Mataifa una wasiwasi kuwa ucheleweshwaji wa njia yoyote wa kura hiyo unaweza kuzusha ghasia upya.

Umati wa maelfu kadhaa ya waandamanaji wanaounga mkono kuwepo kwa umoja wa Sudan waliwaandama wananchi wapatao 40 kutoka Kusini waliofika katika mkutano wa hadhara mjini Khartoum.

Polisi nao walijiunga na raia katika kuwapiga wananchi hao wa Kusini, ambao walilazimika kukimbia eneo hilo.

Mvutano

Mwandishi wa BBC mjini Khartoum, James Copnall anasema sakata hilo ni tukio ambalo ni aghalabu kuonekana hadharani, na ni ishara ya kuongezeka kwa mvutano ambao unatishia kuigawa Sudan.

Wakati huohuo, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameutaka ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa kupeleka majeshi ya kulinda amani katika mpaka na upande wa kaskazini kabla ya kura ya maoni.

Kati ya maeneo manane na 10 katika eneo la mpaka, likiwemo eneo la Abyei, bado yana mzozo, na wachambuzi wa mambo wanasema kugombea moja kati ya maeneo hayo kunaweza kuzisha mapambano ya kijeshi. Pande zote mbili zimepeleka wanajeshi wake katika maeneo hayo.

Wanajeshi

Wanadiplomasia hao wamesema ombi la Bw. Kiir litafikiriwa, lakini hakuna ahadi ya uwezekano wa kupelekwa kwa wanajeshi imetolewa.

Ziara ya wajumbe 15 wa Umoja wa Mataifa, ililenga kutazama vita vya wenyewe kwa wenyewe katika jimbo la magharibi la Darfur, na pia kutazama kuchelewa kwa matayarisho ya kura ya maoni, ambayo inatarajiwa kufanyika January 9.

Lakini mwakilishi wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Mark Lyall Grant amewaambia waandishi wa habari mjini Khartoum kuwa wanataka kuona jitihada za kutosha za kumaliza "masuala kadhaa muhimu", kama vile ufadhili na uraia, kabla ya kura ya maoni kufanyika

No comments:

Post a Comment