KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, October 13, 2010

Tsvangirai awakana mabalozi wa Mugabe




Rais Robert Mugabe na Bw Morgan Tsvangirai



Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai amewaandikia viongozi duniani akisema mabalozi wa Zimbabwe hawaiwakilishi serikali yake.

Alisema wawakilishi hao wameteuliwa tu na Rais Robert Mugabe, ambapo Bw Tsvangirai anagawana naye madaraka.

Lakini Bw Tsvangirai alisema hakushauriwa katika uteuzi huo, ambapo anasema inavunja makubaliano ya umoja wa serikali.

Haijajulikana iwapo Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Afrika Kusini itawatambua mabalozi hao.

Hizi ni ishara za mpasuko zilizojitokeza hivi karibuni katika makubaliano ya kugawana madaraka, huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika mwakani.

Wiki iliyopita, Bw Tsvangirai alimshutumu Bw Mugabe kwa kukiuka makubaliano baada ya kuteua wengine wengi bila kumshirikisha.

Msemaji wa Bw Tsvangirai Luke Tamborinyoka aliiambia BBC siku ya Jumanne, "Hao si mabalozi- ni vibaraka wa Zanu-PF."

Lakini alikataa kusema Bw Tsvangirai angependa hatua gani zichukuliwe na serikali za kigeni.

Alisema, "huo ni uamuzi wao".

Bw Tsvangirai alikutana na wanadiplomasia mjini Harare kuelezea msimamo wake.

Pia aliziandikia nchi za Italia, Sweden na Uswizi, kuhusiana na mabalozi wa Zimbabwe katika nchi hizo.

Kiongozi wa Movement for Democratic Change hivi karibuni alilalamika juu ya vurugu zilizofanywa wakati wa mikutano ya umma wakikusanya maoni ya katiba mpya.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limewashutumu wafuasi wa Zanu-PF kwa kuhusika na mashambulio hayo.

Bw Mugabe na Bw Tsvangirai, ambao wamekuwa wapinzani kwa muda mrefu, wamekubali kugawana madaraka baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2008.

Katika makubaliano ya serikali ya muungano, wanasiasa hao wawili walikubali kutengeneza katiba mpya itakayofuatiwa na kura ya maoni, halafu uchaguzi mpya

No comments:

Post a Comment