KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, October 6, 2010

Mshauri wa usalama wa rais wa Nigeria afutwa kazi





Mshauri wa usalama wa rais wa Nigeria afutwa kazi
Idara ya ujasusi nchini Nigeria SSS imemuachilia huru mwanasiasa mashuhuri aliyekuwa ametiwa mbaroni.

Raymond Dokpesi, mwekezaji katika sekta ya habari vile vile mwanasiasa alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mashambulio ya mabomu wakati wa sherehe za miaka 50 ya uhuru Nigeria.

Huku haya yakiarifiwa naye rais GoodLuck Jonathan amemuachisha kazi mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama kufuatia tukio hilo la wiki iliopita.


Kukamatwa kwa Raymond Dokpesi na shirika la ujasusi la Nigeria kumewashtua wanasiasa wengi nchini humo. Yeye ni tajiri anayemiliki vyombo vya habari na kujulikana na wanasiasa wengi, ikiwa ni pamoja na Rais Goodluck Jonathan.

Hivi majuzi alitangaza kuwa anamuunga mkono mgombea wa urais aliyekuwa rais wa zamani wa Nigeria, Jenerali Babangida.

Kukamatwa kwake kumewashangaza wengi mjini Abuja na baadhi ya marafiki wake wanasema ni vigumu kuamini jambo hilo.

Inafahamika kuwa alihojiwa kuhusu mlipuko wa bomu uliotokea wiki iliopita jijini humo, wakati ambapo Nigeria ilikuwa inaadhimisha miaka hamsini tangu ipate uhuru.

Vyombo vya habari vinasema kuwa ujumbe mfupi kupitia simu ya mkononi unaonyesha uhusiano kati ya Dokpesi na mshukiwa mkuu katika shambulizi hilo, Henry Okah Okah aliyefikishwa mahakamani Afrika Kusini hapo jana kuhusiana na tukio hilo.Dokpesi anatarajiwa kuhojiwa zaidi na idara ya ujasusi hii leo.

Wakati haya yakiarifiwa, Rais Goodluck Jonathan amemfuta kazi mshauri wake wa masuala ya usalama wa kitaifa. Kuna uvumi kuwa alikosa kuchukua hatua licha ya kuwa na taarifa za kijasusi kuhusu shambulio hilo la bomu.

Nafasi yake itachukuliwa na Jenerali Azazi anayetoka eneo la Niger Delta kama rais Jonathan.

Kufutwa kwa mshauri wake na uteuzi si kwa kawaida na inaonekana rais alinuia kumuweka mshirika wake wa karibu kwenye nafasi muhimu ya usalama.

No comments:

Post a Comment