KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, September 2, 2010

Ripoti ya mauaji ya Rwanda bado utata


Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu inasema kuwa uamuzi juu ya tarehe ya kuchapisha ripoti yenye utata kuhusu Afrika ya kati ambayo ingekuwa ni leo, sasa unategemea uamuzi wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Hata hivyo ripoti iliyovuja imezua mtafaruku wa kisiasa nchini Rwanda ambayo imetishia kukwamisha uhusiano wa aina zote na umoja huo endapo ripoti hiyo itachapishwa.

Ripoti hiyo inasema kuwa Jeshi la Rwanda huenda lilishiriki katika mauaji ya kimbari ya Wahutu asilia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwaka 1996 na 1997.


Madai haya ni makali kutokana na siasa za Afrika ya kati, pamoja na sera ya nchi za magharibi kuhusu eneo hilo ambayo ilibuniwa kufuatia mauaji kama hayo na kuidhinishwa na sheria ya kimataifa -mauaji ya kimbari ya kabila la Watutsi yaliyofanywa na Wahutu wa Rwanda mwaka 1994.

Mauaji ya kimbari ya kabila la Watutsi wa Rwanda ya mwaka 1994 yaligeuza siasa za Afrika ya kati ambapo takriban watu milioni moja waliuawa na serikali ya Wahutu wenye msimamo mkali.

Mataifa ya magharibi yalishindwa kuzuia mauaji hayo, yaliyokomeshwa tu baada ya kundi la waasi wa Kitutsi kuingia madarakani.

Mamilioni ya wakimbizi wa Kihutu wakiwemo walioshiriki mauaji ya Watutsi walikimbilia katika nchi jirani ya Congo.

Hili likasababisha mabadiliko katika tarakimu za idadi ya watu na kutonyesha donda la miaka mingi, na hivyo kusababisha kuundwa kwa serikali mpya ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.



Athari



Ripoti iliyovuja inasema kuwa Jeshi la Rwanda lenye idadi kubwa ya Watutsi na mojawapo ya majeshi imara katika eneo hilo, huenda lilishiriki katika mauaji ya kimbari ya Wahutu walio uhamishoni nchini Congo.

Rwanda inaongozwa na aliyekuwa kamanda wa kundi la waasi la Kitutsi aliyeingia madarakani mwaka 1994, Paul Kagame.

Serikali yake inasema kuwa ikiwa umoja wa mataifa utachapisha ripoti hiyo kama ilivyoonekana kwenye ripoti iliyovuja, Rwanda itaondoa vikosi vyake kutoka operesheni za kulinda amani huko Darfur pamoja na kusitisha ushirikiano wowote uliopo na umoja huo.







Wakimbizi wa Rwanda




Lakini athari za kuchapisha ripoti hiyo zinaweza kuzidi hapo. Nchi za magharibi ikiwemo Marekani na Uingereza zimerekebisha sera zao juu ya Rwanda kwa sababu ya kushindwa kuzuia mauaji ya Watutsi ya mwaka 1994.

Ni dhahiri kwamba Rais Paul Kagame anatunzwa kwa mkono wa huruma na nchi za magharibi kutokana na hilo.




Ufaransa kwa upande wake imeshutumiwa na Rais Kagame kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya Watutsi. Na kwa sasa mfumo wa siasa za Afrika ya kati umejengwa kwa kutegemea uwezo wa jeshi la Bw Kagame.


Lakini ripoti hii ya umoja wa mataifa kuhusu mauaji ya kimbari ya Wahutu na kuwa vikosi vya Bw Kagame vilihusika kunaweza kubadili mtazamo wa kizazi kizima, siasa na sera ya eneo zima la Afrika ya kati na kwingineko.

No comments:

Post a Comment