KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Tuesday, September 21, 2010
A Kusini yapambana na wawindaji haramu
Vifaru Afrika Kusini
Watu tisa wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama moja nchini Afrika Kusini siku ya Jumatano kwa madai ya kufanya uwindaji wa vifaru kwa njia isiyo halali.
Washukiwa hao ni pamoja na mfanyabiashara na waganga wawili wa mifugo wanaofanya kazi katika jimbo la Limpopo.
Afisa mmoja ameiambia BBC watu hao wanadaiwa kupeleka pembe za vifaru katika masoko ya Asia.
Zaidi ya vifaru 200 wameuliwa kutokana na pembe zao tangu mwanzo wa mwaka huu.
Pembe za vifaru huuzwa kimagendo na hutumiwa katika baadhi ya nchi za barani Asia kwa ajili ya dawa.
Msemaji wa polisi Kanali Vish Naidoo ameiambia BBC, " Ni hatua kubwa sana kwetu na tunaamini itazuia na utakuwa ujumbe kwa wanaotaka kufanya magendo kwamba shughuli zao zitakwama."
Idadi nyingine ya pembe za vifaru ambayo haijatajwa zilikamatwa huko Musina, katika mpaka wa Zimbabwe na Afrika Kusini, eneo ambalo kundi hilo lilikuwa likifanya kazi.
Kanali Naidoo alisema, washukiwa hao watakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na mauaji, uuzaji na utupaji wa mizoga ya vifaru.
Watu hao waliohusishwa na "matukio mengine mengi" wanatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi huko Musina siku ya Jumatano.
Hivi karibuni Afrika Kusini imezidi kubana sheria zake za uwindaji haramu lakini uhalifu huo unazidi kuongezeka
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment