KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 23, 2010

Wanajeshi wasaidia hospitalini A Kusini

Takriban wafanyakazi wa serikali milioni moja wa Afrika Kusini wanaendelea na mgomo licha ya mahakama kutoa amri ya kuzuia mashirika yao kufunga huduma za dharura.

Polisi wamewafyatulia risasi za plastiki wafanyakazi waliogoma wanaotoa huduma za afya, na kuwajeruhi waandamanaji huko Durban.

Jeshi limesambaza wataalamu wa afya katika hospitali mbalimbali nchini kote ili huduma za dharura ziweze kutolewa.

Vyama vya wafanyakazi vilianza mgomo siku ya Jumatano, vikitaka ongezeko la mshahara.

Siku ya Jumamosi serikali ilitoa amri ya kupinga mgomo huo, ambapo vyama hivyo vilipinga hapo hapo.

Wale waliofyatuliwa risasi za plastiki nje ya hospitali ya Addington mjini Durban waliripotiwa kuziba mlango wa kuingilia wafanyakazi.

Muuguzi Buhle Ntsele, aliyekuwa akitoka damu kwenye paja lake baada ya kupigwa risasi hizo, alisema mgomo wao ulikuwa wa amani.

Shirika la habari la Afrika Kusini (Sapa) limeripoti, " Watu wanaofanya kazi wametusaliti. Tunahitaji kuwashughulikia."

Mugwene Maluleke, msemaji wa chama cha wafanyakazi nchini humo (Cosatu) aliiambia BBC mwishoni mwa juma kuwa wanachama wa chama hicho hawatoshauriwa kurejea kazini.

Chama kimoja cha ziada cha walimu kinatarajiwa kujiunga na mgomo huo.

Serikali imekubali kuongeza mshahara kwa asilimia saba. Vyama vya wafanyakazi vinavyoshirikiana na Cosatu vinadai ongezeko la asilimia 8.6.

Serikali imesema haina uwezo wa kuongeza kiwango hicho ambacho ni mara mbili ya kiwango cha mfumko wa bei.

Rais Jacob Zuma ametetea haki ya vyama hivyo kugoma lakini pia amezisihi kuacha ghasia na vitisho.

No comments:

Post a Comment