KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, August 24, 2010

Wabunge wa Somalia wauawa hotelini

Msemaji wa majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Afrika amesema, Wasomali wenye silaha wamevamia hoteli iliyopo karibu na kasri ya Rais na kuua wabunge katika mapambano yaliyopo siku yake ya pili.

Naibu waziri mkuu aliiambia BBC takriban watu 32 wameuawa katika shambulio hilo.

Mwandishi wa BBC Mohammed Olad Hassan wa Mogadishu alisema watu hao walivaa kama askari wa serikali.

Walivamia hoteli ya Muna, na kumfyatulia risasi mlinzi, na baadae mmoja wao akajilipua ndani ya jengo hilo.

Sheikh Ali Mohamud Rage, msemaji wa wapiganaji wa al-Shabab, alisema wanachama wa "majeshi maalum" walihusika na shambulio hilo.
'Vita vizito'

Uvamizi kwenye hoteli hiyo umefanyika siku ya pili ya mapigano mazito baina ya wapiganaji wa al-Shabab na majeshi ya serikali ya mpito, yanayoungwa mkono na Umoja wa Afrika (AU).

Mwandishi wetu alisema maafisa wa serikali ni maarufu sana katika hoteli hiyo ya Muna, kwasababu iko katika eneo linalodhibitiwa na serikali na usalama ni wa hali ya juu.

Waliojeruhiwa Somalia

Mbali na wabunge sita, maafisa wa serikali watano na raia 21 nao waliuawa.

Meja Barigye Bahoku alithibitisha kuwa ni shambulio la kujitoa mhanga na kusema majeshi ya usalama yalikuwa yakimsaka mtu wa pili aliyekuwa na silaha.

Alisema mtoto mmoja wa miaka 11 aliyekuwa akisafisha viatu na mwanamke mmoja aliyekuwa akiuza chai mbele ya hoteli hiyo ni miongoni mwa waliofariki dunia.

Mbunge mmoja katika hoteli hiyo ya Muna alimwambia mwandishi wa BBC kuwa "maiti zimesambaa kote" na mandhari yalikuwa ya "mauaji ya kinyama".
Kulipiza kisasi

Al-Shabab ilianza mapigano siku ya Jumatatu baada ya msemaji wake kutangaza kuandaa "vita vikubwa" dhidi ya majeshi ya AU, wakiwaelezea wanajeshi hao wa kutunza amani 6,000 kama "wavamizi".

Takriban watu 40 wameuawa katika mapigano hayo na zaidi ya 130 wamejeruhiwa, huku mabomu yakiwa yamerushwa kwenye maeneo waishio raia.

Serikali inadhibiti maeneo machache tu ya mji mkuu wa Somalia.

Kundi hilo lilikiri kuhusika na shambulio la mabomu mawili kwenye mji mkuu wa Uganda wakati wa Kombe la Dunia, likisema kupinga usambazaji wa majeshi ya Uganda nchini Somalia lililopo na Umoja wa Afrika.

No comments:

Post a Comment