KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, August 4, 2010

'Naogopa Kufariki Nisaidieni'


Mwanamke wa nchini Iran ambaye kutokana na kufanya zinaa alihukumiwa kupigwa mawe hadi atakapofariki, amesema kuwa anaogopa kufariki na anaomba awakumbatie watoto wake kwa mara ya mwisho.
"Kila siku kabla ya kulala huwa nafikiria nani ndio angekuwa wa kwanza kunirushia mawe", alisema Sakineh Mohammadi Ashtiani mwenye umri wa miaka 43 ambaye ni mama wa watoto wawili.

Hivi karibuni adhabu ya kuuliwa kwa kupigwa mawe ya Sakineh ilibadilishwa na kuwa adhabu ya kuuliwa kwa kunyongwa baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kuishinikiza serikali ya Iran kumwachia huru mwanamke huyo.

Katika ujumbe wake alioutuma kwa watu toka jela aliyofungwa mjini Tabriz, Sakineh aliwashukuru watu waliofanya kampeni ya kutaka aachiwe huru lakini alisema kuwa anaogopa kufariki.

"Siku niliyohukumiwa kuuliwa ni siku ambayo naiona kama nilidondokea kwenye shimo refu lenye giza, nimepoteza fahamu zangu, siku nyingine kabla ya kulala huwa nafikiria nani angekuwa wa kwanza kunipiga mawe na kwa sababu ipi?, Nawaambieni nyote, Naogopa kufariki naomba nisaidieni, naomba niwakumbatie watoto wangu kwa mara ya mwisho", alisema Sakineh.

Sakineh aliendelea kusema kuwa alivunjika sana moyo siku ambayo alicharazwa bakora 99 mbele ya mtoto wake Sajad mwenye umri wa miaka 17.

Sakineh alipatikana na hatia ya kufanya mapenzi nje ya ndoa yake mwaka 2006 na alihukumiwa kuuliwa kwa kupigwa mawe lakini kutokana na kampeni za mashirika ya kutetea haki za binadamu hatimaye serikali ya Iran hivi karibuni iliibadilisha adhabu hiyo na sasa Sakineh atauliwa kwa kunyongwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu bado yanaendeleza kampeni za kutaka Sakineh aachiwe huru lakini serikali ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa adhabu iliyotolewa itatekelezwa kama inavyotakiwa.

No comments:

Post a Comment