KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, August 4, 2010

Mchakato wa katiba mpya Kenya


Katika muda wa chini ya wiki moja Wakenya watapiga kura ya maoni tarehe 4 Agosti 2010,watapiga kura kukubali au kukataa katiba inayopendekezwa. Kura hii ya maoni ni kilele cha miongo miwili ya harakati za kutafuta katiba mpya.
Yafuatayo ni maswali na majibu kuhusu baadhi ya maswala muhimu katika mchakato huo:
1. Ni lini na kwa nini wakenya wakaanza kutafuta katiba mpya?

Katiba Kenya

Mchakato wa kutafuta katiba mpya ulianzishwa mwaka 1990 na wanasiasa maarufu,viongozi wa kidini na wanachama wa mashirika ya kiraia. Waliteta kuwa katiba iliyopo ilimpa uwezo mkubwa rais wa zamani Daniel arap Moi na kuipa serikali kuu mamlaka yote ya kusimamia raslimali zote. Walitaka mamlaka hayo kupunguzwa na majimbo kupewa mamlaka zaidi ya kusimamia rasilimali zao.
2. Katiba inayopendekezwa ina tofauti gani?

Tofauti kubwa ni mfumo wa utawala:

a)Uteuzi wa mawaziri

Tofauti na mfumo ulioko sasa, katika katiba inayopendekezwa, mawaziri hawatateuliwa kutoka bunge, badala yake watakuwa wataalamu kutoka sekta mbali mbali

b)Mamlaka kwa serikali za majimbo:
* Kutakuwa na mabunge mawili, bunge la kitaifa litakalokuwa na wawakilishi kutoka kwenye majimbo au maeneo bunge na bunge lingine la maseneta.
* Katiba inayopendekezwa itakuwa na majimbo 47 yatakayowakilishwa na maseneta.
* Bunge la senate litakuwa likiwakilisha majimbo, na kujadili ugawanaji wa raslimali katika majimbo

* Magavana watakuwa wakuu wa majimbo

c) Kuwajibisha wabunge:
Kipengele hiki kinatoa fursa kwa wakenya kuwarudisha nyumbani wabunge ambao hawatekelezi wajibu wao.

d) Uraia wa nchi mbili

Tofauti na katiba iliyoko sasa, katiba mpya inayopendekezwa inaruhusu raia wa Kenya kuchukua uraia wa nchi nyingine bila kupoteza uraia wa Kenya.

3. Ni vipengele vipi vilivyoleta utata?
a)ardhi
Ili kutatua suala la kutolewa kwa ardhi na utawala uliokuwepo kwa njia isiyo sawa, katika katiba inayopendekezwa ardhi zilizopatikana kwa njia isiyo halali hazitalindwa kisheria na hivyi zinaweza kuchukuliwa na serikali.
b)Dini
Kama ilivyo sasa,katiba inayopendekezwa pia itakuwa na mahakama za waislamu maarufu kama mahakama za kadhi.Mahakama hizo zimekuwepo tangu wakati wa kupata uhuru lakini baadhi makanisa ya kikristo yalitaka mahakama hizi ziondolewe wakidai kuwa kuziweka katika katiba ni kupendelea dini moja. Mahakama hizo zinatatua kesi za kijamii na ndoa kati ya waislamu.
c)Haki ya msingi:Uavyaji mimba

Moja ya maswala ambayo yameleta utata kati ya viongozi wa dini na wanasiasa ni kipengele ambacho baadhi ya viongozi wa dini wanadai kinaandaa mazingira kwa watu kuavya mimba,lakini je kipengele hicho kinaruhusu uavyaji mimba?

· Haki za msingi sehemu ya 2 kifungu 26(4) inasema:
‘Uavyaji mimba hauruhusiwi, ila tu iwapo mtaalamu wa afya atabaini kuwa maisha ya mama mja mzito yako hatarini,au kulingana na mwongozo utakaotolewa na sheria zengine.’

Wanasema kuwa hali hii inatoa mwanya kwa watu kuavya mimba.
d)Wanawake
Kuna vifungu vinavyowapa fursa zaidi za uwakilishi wanawake:

Wajumbe 47 kati ya 350 katika bunge la taifa watakuwa wanawake watakaoteuliwa kutoka kila jimbo
Wajumbe 16 kati ya 67 wa bunge la seneti watakuwa wanawake watakaoteuliwa na vyama vya siasa
4. Nani anaongoza kundi gani?

Katiba Kenya

NDIO
Rais Mwai Kibaki
Katika siku za hivi karibuni ameongeza kasi yake ya kufanya kampeini za kuunga mkono mapendekezo ya katiba,ikiwa itapitishwa itakuwa sifa kubwa kwa utawala wake. Aliahidi kuwa katiba mpya ingepatikana katika muda wa siku 100 alipochukua madaraka mwaka 2003.
Waziri mkuu Raila Odinga
-Amekuwa katika harakati za kutaka mabadiliko kwa muda mrefu, amekuwa akiongoza kampeini za kundi la NDIO hadi alipokuwa mgonjwa wiki 3 zilizopita.

HAPANA
Rais mstaafu Daniel Moi
Anasema katiba hiyo ni mbaya,hasa vipengee kuhusu ardhi ambavyo anasema vitaleta mgawanyiko na vurugu nchini Kenya. Moi ni miongoni mwa wakenya wenye kumiliki sehemu kubwa ya ardhi.Baadhi ya viongozi wa kikristo
Wanateta kuwa katiba hiyo inaruhusu uavyaji mimba

Waziri wa elimu ya juu William Ruto
Ni mbunge muasi wa chama cha waziri mkuu Raila Odinga. Anasema katiba inayopendekezwa itawagawanya wakenya kwa misingi ya kikabila na kidini

No comments:

Post a Comment