KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, August 12, 2010

Matokeo ya muda yatangazwa Rwanda

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Rwanda imetangaza matokeo ya muda ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumatatu wiki hii.

Katibu mtendaji wa tume ya taifa ya uchaguzi huo Charles Munyaneza alisema mgombea wa RPF Paul Kagame alichaguliwa kwa asilimia 93 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani wake wa karibu Dr Jean Dascene Ntawukuriryayo ameshika nafasi ya pili akiwa na asilimia 5, Prosper Higiro amepata asilimia 1.3 naye Dr Alivera Mukabaramba amepata asilimia 0.4 ya kura.

Tume ya taifa ya uchaguzi imesema mgombea yeyote anayepinga matokeo hayo ana muda wa saa 48 kupeleka malalamiko yake kabla ya tume hiyo kuidhinisha na kuyatangaza rasmi.

Lakini haitarajiwi kuwepo malalamiko yoyote kwani wagombea wengine wamekubali kushindwa na kutoa risala za pongezi kwa mshindi Rais Paul Kagame.

Haya ni matokeo ambayo kwa sehemu kubwa yalikuwa yanatarajiwa na watu wengi ambao mwanzoni mwa mchakato mzima wa uchaguzi hawakuwaona wapinzani wa Rais Kagame kama watu wanaoweza kumtikisa.

Dhana hiyo hasa ilitokana na vyama vyao kuwa washirika wa karibu na chama tawala RPF kilichowashirikisha katika utawala wake tangu kilipotwaa madaraka mwaka 1994, ambapo wengine waliwaona kama wapambe wa kuonyesha tu kwamba upinzani upo.

Lakini wao wanahakikisha kuwa vyama vyao vimekomaa kisiasa kiasi cha kutokukubali tena kubebwa na chama tawala na ndiyo maana waliamua kusimama katika uchaguzi huu.

No comments:

Post a Comment