Akiwa na umri wa miaka 18 kijana mmoja wa nchini Marekani alihukumiwa kwenda jela miaka 75 kwa kosa la ubakaji lakini baada ya kutumikia miaka 27 ndani ya jela, aliachiwa huru ijumaa baada ya kugundulika kuwa hakutenda kosa hilo.
Michael Anthony Green aliingia jela akiwa na umri wa miaka 18 na alitoka jela ijumaa akiwa na umri wa miaka 44 huku akiwa amegubikwa na hasira kali za kutumikia miaka 27 jela kwa kosa ambalo hakulifanya.
Green alilakiwa na ndugu zake takribani 20 ambao waliambatana na watoto wao waliozaliwa wakati Green akiwa jela.
Alipoulizwa atafanya nini sasa baada ya kuachiwa huru, Green alisema "Nitaanza maisha upya".
Green alitoka jela kufuatia juhudi yake ya kuwatumia barua wanasheria na meya barua za kuomba kesi yake irudiwe upya.
Hatimaye kesi yake ilianza kusikilizwa tena mwaka 2008 baada ya mwanasheria mkuu mpya wa eneo hilo kuingia madarakani na kuamua kuifuatilia kesi hiyo.
Mwaka 1983, wanaume wanne walimteka mwanamke toka kwenye kibanda cha simu na kumpeleka kichakani ambako watatu kati yao walimbaka mwanamke huyo.
Wanaume hao walimtelekeza mwanamke huyo na kutoroka na gari lakini baada ya taarifa kuwafikia polisi, polisi walianza kulifukuza gari lao na kupelekea wanaume hao walitelekeze njiani na kukimbia vichakani. Green alinaswa na polisi wakati akikatiza kwenye kichaka ambacho polisi walikuwa wakiwatafuta wabakaji hao.
Mwanamke aliyebakwa hakuweza kumtambua Green kama mbakaji wake wakati Green alipoletwa mbele yake lakini baadae aliichagua picha ya Green alipoonyeshwa picha za watuhumiwa mbalimbali. Green alihukumiwa kwenda jela miaka 75 akiwa ndiye mtuhumiwa pekee wa kesi hiyo aliyefikishwa mahakamani.
Wakati kesi hiyo ikirudiwa tena kuanzia mwaka 2008, kielelezo pekee cha kesi hiyo kilikuwa ni nguo zilizokuwa zimevaliwa na mwanamke aliyebakwa siku aliyobakwa. Uchunguzi wa DNA ulionyesha kuwa Green hakuhusika katika ubakaji.
Wapelelezi walifanikiwa kuwapata wabakaji halisi wa mwanamke huyo lakini wote waliachiwa huru kwakuwa miaka mingi sana ilikuwa imepita na sheria haziruhusu kufunguliwa kwa shitaka la ubakaji baada ya miaka mingi sana kupita.
Huku akiwa ameshikilia picha ya mama yake ambaye alifariki wakati yeye akiwa jela, Green alisema "Sijui kama nitaweza kuwasamehe polisi".
No comments:
Post a Comment