KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 16, 2010

Askari wawili wa UNAMID watekwa nyara Sudan


Vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan vimesema askari wake wawili wametekwa nyara.

Kikosi hicho cha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika (UNAMID), kimesema washauri wawili wa polisi walitekwa nyara na watu wenye silaha wakiwa ndani ya gari karibu na makaazi yao yaliyoko Nyala, Darfur Kusini.

Msemaji wa UNAMID, Chris Cycmanick alisema lengo la shambulizi hilo halijabainika.

Hadi sasa UNAMID haijawasiliana na watekaji nyara.

Kumekuwa na visa kadhaa vya utekaji nyara katika jimbo la Darfur katika miezi kumi na nane iliyopita, tangu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutoa hati inayoagiza kukamatwa kwa Rais wa Sudan, Generali Omar el Bashir.

Visa vingi vya utekaji nyara ni kwa ajili ya kutafuta fedha ya kikombozi.
Kuzorota uhusiano kati ya UNAMID na serikali

Kikosi cha UNAMID kinakabiliwa na wakati mgumu. Serikali ya Sudan inataka kikosi hicho kiwakabidhi kwa serikali viongozi sita wa Darfur, ambao walipewa hifadhi na kikosi hicho cha kimataifa, kufutia ghasia katika kambi ya wakimbizi ya Kalma.

Watu hao sita wanashtumiwa kwa kuchochea ghasia ambazo zilisababisha watu kadhaa kuuwawa.

Baadhi ya maafisa wa Sudan wamezungumzia hata kuwafurusha wanajeshi wa kulinda amani, ikiwa hawatowakabidhi watuhumiwa.

Mratibu Mkuu wa huduma za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa,John Holmes, ameishtumu serikali ya Sudan kwa kuzuwia misaada iwafikie wakimbizi katika kambi ya Kalma tangu mzozo huo uanze.

Lakini gavana wa Darfur Kusini anakanusha madai hayo.

UNAMID ilipeleka kikosi chake mwaka wa 2008 ili kulinda raia na kuimarisha usalama wa Darfur.

No comments:

Post a Comment