KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, August 2, 2010

Ajali ya boti yaua zaidi ya 70 Uganda


Kuna hofu kwamba watu 73 wamefariki dunia baada ya mashua waliokuwa wakisafiria kuzama katika ziwa Albert usiku wa Jumamosi nchini Uganda.

Ajali hii ilitokea eneo lijulikanalo kama Kakoma katika kijiji cha Runga, Wilaya ya Hoima.

Polisi ilisema kuwa imeokoa watu 17 huku maiti za mwanamke mmoja na watoto wanne zimeopolewa.

Mashua hiyo ilikuwa safarini kutoka Hoimo kuelekea soko la Panymur katika Wilaya ya Nebbi, mwendo wa saa nane.

Miongoni mwa abiria waliokuwa kwenye mashua hiyo ni wafanyabiashara kutoka maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Hoima wakiwemo watoto wa shule, tani kadhaa za samaki na mizigo.

Kwa mujibu wa mtu mmoja aliyeokoka, mashua hiyo iliyoanza safari yake majira ya usiku wa Jumamosi ilikuwa ikiongezea abiria katika kila kituo.

Abiria mwingine alisema kwenye majira ya saa tatu usiku , alionya abiria kuwa kuna kimbunga kitakachotokea na kuwaomba baadhi ya abiria washuke.

Alijaribu hata kuwarejeshea nauli lakini wakamuomba aendelee na safari pamoja na abiria wote.

Afisa mkuu wa kituo cha Polisi mjini Hoima, Romeo Ojara amesema ajali hiyo ilisababishwa na mizigo na abiria wa kupindukia.

Taarifa za awali zilionyesha kuwa mashua hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 90 huku ikiwa na uwezo wa kuchukua abiria 40.

No comments:

Post a Comment