KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, July 27, 2010

Uingereza yashtakiwa kwa madini ya Kongo


Shirika lijulikanalo kama Global Witness linasema linaishitaki Uingereza kwa kushindwa kuyafahamisha makampuni yanayoendesha biashara ya madini yenye utata kutoka Congo yaliyopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa.

Shirika hilo limekwenda kwenye mahakama kuu kutathmini hoja yake kwamba serikali ya Uingereza inakiuka majukumu yake kisheria.

Ikumbukwe kuwa juhudi za kimataifa zinafanywa kuzuia biashara ya madini kutoka katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi wenye silaha.

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema ilitarajia kampuni za Uingereza zingetumia busara zao kuendesha biashara kwa uangalifu.

Waasi wanadhibiti madini kama dhahabu, bati na ya coltan katika nchi ambako raia wake milioni tano wameuawa kati ya mwaka 1996 na 2003 wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na athari zilizofuata.

Maazimio ya Umoja wa mataifa yaliyopitishwa mwaka 2008 na 2009 yaliweka vikwazo vya kusafiri na kutia tanji kwa kampuni zozote zinazounga mkono biashara hiyo haramu.

'Kukataa kuchukua hatua'
Global Witness pamoja na kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa linasema lina ushahidi wa kutosha kwamba kampuni za Uingereza zimeunga mkono makundi ya wapiganaji kwa kununua madini kutoka maeneo ya waasi hao.

Mkurugenzi anayehusika na kampeni katika Global Witness Gavin Hayman, anasema makundi hayo hutumia fedha za madini kwa kununulia silaha na kuanzisha fujo dhidi ya raia.

Maazimio ya Umoja wa Mataifa yalibaini kuwa makampuni yanayoendesha biashara hiyo ya madini moja kwa moja kutoka kwa wapiganaji ni sehemu ya tatizo.

"Lakini pamoja na kuiomba mara nyingi kujiepusha na biashara hiyo, serikali ya Uingereza imekataa kuchukua hatua, na kutuacha bila njia nyingine ila kwenda mahakamani.''

Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imesema haiwezi kutoa maelezo mengi kuhusiana na kashfa hii.

Taarifa yake imesema, serikali ya Uingereza inategemea kampuni zote za Uingereza zinazoendesha biashara katika Jamhuri ya Congo kufanya hivyo kwa tahadhari na kutumia viwango vya juu vya busara, na kutumia juhudi za kubaini njia ambazo madini hayo yamepatikana.

Nia yetu kuu, alisema msemaji wa mambo ya nje ni kuona maliasili yote ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikidhibitiwa na dola.

Tunaendesha miradi kadhaa huko ili kubuni uongozi bora wa madini ya nchi hiyo, tukidhamiria kuimarisha uhusiano wetu katika maeneo haya.

No comments:

Post a Comment