KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Monday, July 26, 2010
Sarkozy alaani mauaji ya mateka
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amethibitisha kifo cha mateka mmoja raia wa Ufaransa aliyeuliwa na wanaodaiwa kuwa wapiganaji wa al-Qaeda kaskazini- magharibi mwa Afrika.
Bw Sarkozy amelaani mauaji ya Michel Germaneau mwenye umri wa miaka 78 kuwa "jambo la kuchukiza" akisema mauaji hayo lazima yachukuliwe hatua thabit.
Awali kiongozi wa al-Qaeda katika tawi la magharibi (AQIM) alisema Bw Germaneau aliuawa ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi baada ya mpango wa kumwokoa uliposhindwa.
Wiki iliyopita Ufaransa ilisema ilitoa msaada wa vifaa kwa ajili ya kufanya uvamizi huko Mali.
Bw Sarkozy alisema, "Nalaani vitendo hivi vya kikatili, kitendo hichi kinachukiza, kilichosababisha kifo cha raia asiye na makosa aliyetumia muda wake mwingi kusaidia watu."
Amewasihi pia watu wa Ufaransa kutosafiri kwenye maeneo ya Sahel ikiwemo Mali, Mauritania na Niger.
Bw Germaneau, mhandisi aliyestaafu, alitekwa nchini Niger mwezi Aprili.
Kiongozi wa AQIM Abdelmalek Droukdel alisema katika taarifa iliyorushwa na al-Jazeera kwamba Bw Germaneau aliuliwa katika hatua ya kulipiza kisasi baada ya wapiganaji sita kufariki dunia.
Katika taarifa iliyotolewa kufuatia shambulio la Alhamis, wizara ya ulinzi ya Ufaransa ilisema al-Qaeda katika tawi la magharibi "ilikataa kuthibitisha iwapo alikuwa hai au kufanya majadiliano kumwachia ndugu yetu Michel Germaneau."
Taarifa hiyo ilisema, Ufaransa ilitoa msaada wa vifaa na ufundi kwa majeshi ya Mauritania kufanya shambulio nchini Mali.
Pia ilisema harakati hizo "ziliweza kupunguza nguvu za magaidi hao na kuzuia mpango wa mashambulio dhidi ya waliolengwa huko Mauritania."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment