KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, July 28, 2010

Rais Kibaki amtaka mtangulizi wake kutopinga mageuzi

Huku kampeini za kura ya maoni dhidi ya rasimu ya katiba mpya nchini Kenya zikipamba moto Rais Mwai Kibaki amemkosoa vikali mtangulizi wake Daniel Arap Moi kwa kuendeleza kampeini za kupinga rasimu hiyo.

Akiongea katika mkutano wa kupigia debe katiba kielelezo Mashariki mwa Kenya, Kibaki bila kutaja jina alisema baadhi ya watu wanaopinga katiba wanajiabisha na wamejawa na woga kuona Kenya ikipata katiba mpya.

Kwa maneno yake Kibaki alisema katika mhadhara huko Kirinyaga,''Wazee wengine wanazunguka wakisema katiba ni mbaya.... Ni aibu kubwa kwa wazee kama hawa. Awache wasi wasi na aungane na sisi tupitishe katiba''.

Hii ndiyo mara ya kwanza Rais Kibaki amemkosoa hadharani mtangulizi wake Bw.Moi tangu kuchukua hatamu za uongozi kwa miaka saba sasa.Kibaki japo hakuonekana na ghadhabu yeyote wakati akitoa matamshi hayo alimsihi Moi kuachana na kampeini zake kupinga katiba mpya ili aweze kupata heshima kwa raia wa Kenya.

Wadadisi wanasema Moi ndiye kiongozi aliyestaafu Afrika ambaye ameendelea kuwa na kasi ya kupiga siasa. Katika kura ya maoni iliyopita dhidi ya katiba mpya mwaka 2005, Moi alijiunga na mrengo wa chungwa ambao ulipinga rasimu ya katiba.

Msimamo wa Moi juu ya mageuzi ya katiba haujabadilika na kwa wakati huu ameweza kufadhili kampeini kali nchini Kenya ambapo ameungana na mrengo wa rangi nyekundu unaopinga katiba kielelezo.

No comments:

Post a Comment