KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, July 27, 2010

'Polisi wauaji' mahakamani Misri

Kesi ya polisi wawili wa Misri wanaoshtakiwa kwa kufanya ukatili na kusababisha kifo cha mtu mwenye umri wa miaka 28 mwezi mmoja uliopota imeanza leo.

Khaled Said alikufa akiwa mikononi mwa polisi katika mtaa mmoja huko Alexandria mwezi Juni. Kesi hiyo imesababisha hasira kubwa nyumbani na nje.

Watetezi wa haki za binadamu wameandamana nje ya mahakama huku polisi wakiwa wameweka ulinzi mkali.


Maandamano Misri


Mashahidi wanasema Bw Said alifariki dunia baada ya kuburutwa kutoka kwenye mgahawa na kupigwa. Serikali inasema alimeza paketi ya dawa za kulevya na kupaliwa.

Taarifa kutoka shirika la kimataifa la Amnesty lililotolewa Jumatatu ilielezea wasiwasi kuwa mashahidi katika kesi hiyo wanaweza kuteswa na kuisihi serikali iwahakikishie usalama.



Marekani, Umoja wa Ulaya na makundi mengine ya kutetea haki za binadamu yote yametoa wito wa kufanywa uchunguzi wa wazi.

Ulinzi wa mashahidi
Polisi- afisa anayetoa hati za kukamatwa Mahmoud Salah na Sgt Awad Ismail Suleiman- wanashtakiwa kwa kumkamata mtu huyo kinyume cha sheria na kutumia nguvu nyingi.

Hawakabiliwi na mashtaka ya mauaji.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 28 alifariki dunia Juni 6 katika mji wa Alexandria.

Picha zimesambazwa kwenye intaneti zikimwonyesha akiwa amejaa majeraha, huku taya na meno yake yakiwa yamevunjika.

Hata hivyo, uchunguzi wa mwili wake uliofanywa mara mbili na serikali umeonyesha kuwa alikufa kwa kukosa pumzi baada ya kumeza pakiti ya dawa za kulevya.

Familia yake imeviambia vyombo vya habari vya Misri kuwa awali Bw Said aliweka video inayowaonyesha polisi wawili wakigawana dawa hizo walizozikuta kwenye msako.

Kumekuwa na maandamano kadhaa mjini Cairo na Alexandria, ikiwemo moja iliyohudhuriwa na aliyekuwa mkuu wa masuala ya kinyukilia wa umoja wa mataifa Mohamed ElBaradei.

Shirika hilo la Amnesty limesema, " Iwapo haki inatakiwa kutendekea katika kesi hii, serikali ya Misri lazima ihakikishe wale walioshuhudia mateso hayo pamoja na familia ya marehemu na wale wanaotaka kutoa ukweli wanalindwa kutokana na vitisho na ghasia, na wajihisi wako huru kutoa ushahidi."

Mama yake Said, dada na ndugu wengine walifika mahakamani, lakini familia hiyo haikutoa kauli yeyote.

No comments:

Post a Comment