KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 3, 2010

Padri wa Rwanda akamatwa Uganda

Polisi wamesema, padri wa Rwanda anayeshutumiwa kusaidia kupanga mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi yake ya asili ameshikiliwa nchini Uganda.

Jean-Bosco Uwinkindi alikamatwa baada ya kuingia Uganda ya magharibi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Bw Uwinkindi alishtakiwa mwaka 2001 na mahakama inayoungwa mkono na umoja wa mataifa inayoshughulikia mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu.


Takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuliwa na wanamgambo wa Kihutu katika mauaji ya siku 100 mwaka 1994.
Uchinjaji kanisani

Mauaji ya kimbari Rwanda

Polisi ya Uganda ilitangaza siku ya Ijumaa kuwa Bw Uwinkindi aliwekwa rumande siku ya Jumatano.


Polisi wamesema mshukiwa huyo alisakwa kwa siku mbili kabla ya kutiwa kizuizini.

Gazeti la Daily Monitor limeripoti kuwa Bw Uwinkindi aliingia Uganda kwa kutumia jina tofauti na alikuwa akijaribu kununua ardhi ili aweke makao yake hapo.
Kushtakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu kwa Rwanda (ICTR) inasema Bw Uwinkindi alikuwa mchungaji katika kanisa la Pentekosti karibu na mji mkuu wa Rwanda, Kigali mwaka 1994.

Anashutumiwa kwa kuamuru kuuawa kwa Watutsi, wakiwemo wanawake na watoto, baada ya kuomba hifadhi kwenye kanisa lake.

Waendesha mashtaka wanadai uchunguzi uliofanyika baada ya mauaji ya kimbari, takriban maiti 2,000 zilipatikana karibu na kanisa hilo.
Mpaka alipokamatwa, Bw Uwinkindi alikuwa miongoni mwa washukiwa 11 waliokuwa wakisakwa na ICTR.

Marekani iliahidi kutoa zawadi ya dola za kimarekani milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake. Haijfahamika wazi iwapo kuna yeyote atakayedai zawadi hiyo nono.

Elly Womanya, naibu mkurugenzi wa ofisi ya upelelezi ya Interpol mjini Kampala, amesema mshukiwa huyo atapelekwa ICTR Arusha, Tanzania, haraka iwezekanavyo.
Bw Uwinkindi ni mshukiwa wa pili anayehusishwa na mauaji ya kimbari Rwanda kukamatwa Uganda katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja.Mwezi Oktoba 2009, Idelphonse Nizeyimana, aliyekuwa mkuu wa upelelezi mwenye asili ya Kihutu, alikamatwa mjini Kampala.

No comments:

Post a Comment