KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, July 3, 2010

Nkurunziza wa Burundi aibuka mshindi

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, ameibuka mshindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo Jumatatu wiki hii.

Bw Nkurunziza amejipatia asilimia 91.6 ya kura zote na hivyo ataiongoza Burundi kwa muhula wa miaka mitano ijayo.

Matokeo hayo hayakuwashangaza wengi kwani Rais Nkurunzia alikuwa mgombea pekee wa wadhifa huo katika kinyanganyiro hicho.

Hatua hiyo ni baada ya muungano wa vyama 12 vya upinzani kususia uchaguzi huo kwa madai ya kutaka uchaguzi wa madiwani uliofanyika tarehe 24 Mei mwaka huu urudiwe.

Katika uchaguzi huo chama tawala cha CNDD-FDD kilijipatia ushindi wa kishindo wa asilimia 64, na kuwepo tofauti kubwa kati yake na chama kilichoshikilia nafasi ya pili cha FNL ambacho ni chama kikuu cha upinzani kilichopata asilimia 14.

Kutokana na matokeo hayo upinzani ulidai uchaguzi huo uligubikwa na wizi wa kura na kutaka urudiwe na tume huru ya uchaguzi ijiuzulu.

Hata hivyo, madai yote hayo yalitupiliwa mbali na tume hiyo na ndipo upinzani ukaamua kususia uchaguzi huo wa rais na kujiondoa katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Uchaguzi huu wa rais utafuatiwa na uchaguzi wa wabunge ifikapo tarehe 23 Julai.

Vyama vya upinzani vilishatoa taarifa ya kutotambua matokeo ya uchaguzi huu na pia kuahidi kutoshiriki katika uchaguzi huo ujao wa wabunge.

Lakini vitishio hivyo huenda visitikise sana kwani vyama vingine zaidi ya 10 miongoni mwa vyama zaidi ya 30 vilivyosajiliwa vimetangaza utashi wao wa kushiriki katika uchaguzi huo.

Na tume huru ya uchaguzi, Ijumaa hii imetangaza kwamba vyama hivyo vimeshawasilisha fomu zao za maombi ya usajili.

Miongoni mwa vyama vitakavyogombea viti bungeni ni chama kikongwe cha kisiasa cha Uprona, kilichoiongoza Burundi kwa takriban miaka 30, yaani tokea uhuru wake mwaka 1962 hadi mwezi Juni mwaka 93. Chama hiki kilikuwa kimejiondoa katika uchaguzi wa Rais.

Pamoja na malalamiko ya upinzani, jumuiya ya kimataifa imeupongeza uchaguzi huo wa rais pamoja na ule wa madiwani kwamba ulifanyika katika hali ya kuridhisha na kuheshimu misingi ya kidemokrasia licha ya kutoa kasoro ndogo.

Ila jumuiya hiyo ya kimataifa inatiwa wasiwasi na vitendo vya ulipuaji maguruneti vilivyoibuka kufuatia uchaguzi wa madiwani na kuwakamata wafuasi wa upinzani.

No comments:

Post a Comment