KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Monday, July 26, 2010

Museveni atoa wito Al Shabaab wafyekwe


Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametoa wito wa kufanyika juhudi za pamoja za kimataifa kufyeka kikundi cha wanamgambo wa Kiislamu cha Al Shabaab huko nchini Somalia.

Akifungua mkutano wa viongozi wa Afrika unaofanyika mjini Kampala, Bwana Museveni amesema ni lazima makundi ya wanamgambo yafyekwe barani Afrika, majuma mawili baada ya mashambulizi ya mabomu katika mji huo yaliyowauwa watu wasiopungua 70.

Kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia kijulikanacho kama AMISOM kinajumuisha wanajeshi kutoka Uganda na Burundi.

Wakati huo huo, Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika ameushtmu Umoja wa mataifa kwa kumshtaki Rais wa Sudan Omar Al- Bashir.

Bw Mutharika ambaye ni mwenyekiti wa sasa hivi wa Umoja wa Afrika amesema hoja ya kukamatwa kwa Rais huyo wa Sudan, iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC, inahujumu mshikamano, amani na usalama barani Afrika.

Rais Bashir haudhurii mkutano huo. Anakabiliwa na waranti ya kumkamata akiingia katika nchi mwanachama wa mahakama ya ICC.

Serikali ya Sudan haijatuma mwakilishi kwenye mkutano huo, lakini duru za Sudan zinasema hoja ya kukamatwa kwa Rais Bashir sio sababu ya nchi kukosa uwakilishi, lakini ni kutokana na tofauti za rais huyo na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Viongozi hao wa Afrika wanakutana mjini Kampala huku usalama ukiwa umeimarishwa na idadi kubwa ya maafisa wa usalama.

Walinyamaza kimya kwa muda wa dakika mbili kuwakumbuka watu waliouwawa tarehe 11 Julai kwenye milipuko ya mabomu yaliyolenga mashabiki wa soka waliokuwa wakitazama miochuano ya Kombe la Dunia katika mgahawa mmoja, na pia katika uwanja wa michezo.

Kwenye hotuba yake, Rais Museveni alisema mashambulizi hayo yataharibu zaidi hali ya kundi la Al Shabaab.

Mwandishi wa BBC anasema kuna wasi wasi kwamba mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Al Shabaab huenda yakasababisha vifo vya raia wasio na hatia, na kufanya vikosi vya Umoja wa Afrika kuchukiwa na umma nchini Somalia.

Mzozo wa Somalia umeghubika mkutano huo wa viongozi wa Afrika, ambao mada kuu ilitakiwa kuwa ''Afya ya mama ya uzazi na mtoto pamoja na Afya na Maendeleo ya mtoto.''

No comments:

Post a Comment