KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Wednesday, July 21, 2010
Maadhimisho ya jaribio la kumuua Adolf Hitler.
Wajerumani leo wanau adhimisha mwaka wa 66 tokea kufanyika jaribio la kumwuua kiongozi wa mafashisti Adolf Hitler.
Wanasiasa na viongozi wa kidini walikuwa miongoni mwa walioshiriki katika maadhimisho hayo mjini Berlin.
Siku kama ya leo mnamo mwaka wa 1944 afisa wa jeshi kanali Claus Schenk Graf von Stauffenberg alijaribu kumwuua kiongozi wa utawala wa mafashisti Adolf Hitler kwa kutega bomu chini ya meza katika handaki la Hitler. Lakini Hitler alinusurika jaribio hilo. Kanali Stauffenberg na wenzake walioshiriki katika njama hizo walikamatwa na kuuawa kwa kupigwa risasi mjini Berlin siku moja tu baada ya kufanyika jaribio hilo.
Katika maadhimisho ya kuwakumbuka mashujaa hao waziri wa ulinzi wa Ujerumani Karl -Theodor von Guttenberg amesema leo mjini Berlin kwamba hata katika nyakati za giza na udikteta nchini Ujerumani palikuwapo na Ujerumani ya aina nyingine-Ujerumani bora.
Akitetea maadili ya uhuru, amani na demokrasia waziri zu Guttenberg amesema kuwa maadili hayo lazima yalindwe ikiwa itabidi.
Amesema inabidi kutambua kwamba uhuru,amani demokrasia na utawala wa kikatiba siyo mambo yanayojileta wenyewe.
Ikiwa itabidi maadili hayo lazima yalindwe amesema waziri huyo.Waziri zu Gutteberg amesema maafisa waliokula njama za kumwangamiza Hitler hawakuwa watu waliotoka sayari nyingine bali walikuwa binadamu waliokuwa na nguvu na udhaifu vilevile.
Mwanasiasa huyo ameeleza kuwa watu hao - wapinga ufashisti waliuweka kando woga na kuchukua hatua na walitoa kauli kwa lengo la kuuangusha utawala wa fashisti Hitler.
Afisa Claus Schenk Graf von Stauffenberg na wenzake waliokula njama za kumwuua Adolf Hitler walikamatwa baada ya jaribio kushindikana na walipewa adhabu ya kifo kwa kupigwa risasi mahala ambapo leo ni pa kumbukumbu mjini Berlin.
Watu karibu alfu tatu waliuawa kwa kupiwga risasi na utawala wa mafashisti.
Spika wa baraza kuu la shirikisho la Ujerumani , Jens Böhrnsen aliweka shada la maua mahala hapo katika ishara ya kuwakumbuka maafisa hao na watu wengine
Meya wa jiji la Berlin Klaus Wowereit ambae pia alishiriki katika maadhimisho ya leo amesema harakati za wapinga ufashisti hazikuwa kazi bure.Amesema harakati hizo zimeacha kipimo cha maadili.
Watu kadhaa ambao ni vizazi vya waliokuwa wapinga ufashisti pia walishiriki kwenye maadhimisho ya leo mjini Berlin.
Mwandishi/Mtullya Abdu/AP/ZPR.
Mhariri/Abdul-Rahman
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment