KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, June 8, 2010

Tanzania kuikirimu Brazil leo


Mashabiki zaidi ya 60,000 watakuwa wanagombea kuingia uwanja wa Taifa jijini Dar Es Salaam kushuhudia mchezo wa kirafiki wa kihistoria kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, na Brazil Jumatatu jioni.

Brazil waliwasili Dar Es Salaam Jumapili usiku bila golikipa wao namba moja Julio Cesar, lakini wachezaji wengine nyota kama Kaka, Robinho na Lucio waliwasili na wanategemewa kucheza. Mabeki tegemeo wa Tanzania, Nadir Haroub na Shadrack Nsajigwa wanasema hawatishiki na majina.

“Tofauti na timu za Afrika, timu za Ulaya na za Amerika zinatoa nafasi kucheza, hazikabi sana, hivyo hii mechi ya Brazil itakuwa nzuri kwani tutacheza vizuri,” Haroub alieleza BBC.

“Tumecheza na Ivory Coast na Cameroon na kuweza kuwazuia kwa kiasi fulani. Tutacheza na Brazil kwa kujiamini, na siyo kwamba tunaenda kufungwa tu,” alisema Nsajigwa.

Naye kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo kutoka Brazil, alisema kuwa anawajua vyema Brazil hivyo atatumia mbinu zinazofaa kuwazuia. “Lazima tuwazuie kumiliki mpira au kushambulia kwa kupitia katikati. Sijui matokeo yatakuwa vipi, kwasababu mpira siyo hisabati, lakini nategemea tutaonyesha mchezo mzuri na kudhihirisha kiwango cha Tanzania,” aliongeza.

Brazil itakuwa ndiyo nchi pekee ambayo imecheza mechi za majaribio zaidi ya moja barani Afrika kati ya nchi zote zilizofuzu kucheza Kombe la Dunia. Kabla ya kuja Tanzania, ilicheza mechi ya kwanza wiki moja iliyopita dhidi ya Zimbabwe na kushinda 3-0.

Kiingilio
Viingilio vya mchezo huo ni kati ya Shilingi 30,000 (dola 30) na 200,000 (dola 200), kiasi ambacho ni cha juu sana kuwahi kutozwa katika mechi yoyote Tanzania na mashabiki wamekuwa wakilalamika kuwa kisasi hicho ni kikubwa mno.

Serikali imebidi inawe mikono kwa kutangaza kuwa haikuhusika kupanga viingilio na kwamba vimepangwa na chama cha soka, yaani TFF, ili kufidia gharama za kuwaleta nyota hao wa Brazil.

Magazeti ya Tanzania yamekuwa yakiandika kuwa Brazil wamelipwa shililingi bilioni tatu (takriban dola milioni 3) na TFF hawajakanusha wala kukubali.


Waziri wa Habari na Michezo, George Mkuchika, alisema kuwa TFF walikopa fedha hizo benki na serikali haikuingia gharama zozote na TFF wanaamini kuwa watarudisha gharama kutokana na mauzo ya tiketi.

No comments:

Post a Comment