KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, June 7, 2010

Mkuu wa polisi wa Congo asimamishwa kazi

Mkuu wa polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesimamishwa kazi kufuatia kifo cha mwanaharakati wa haki za kibinadamu.

Waziri wa mambo ya ndani wa Congo amesema maafisa wengine watatu wa jeshi la polisi wametiwa mbaroni, na rais wa nchi hiyo ameamua kushughulikia kesi hiyo.

Floribert Chebeya, mkuu wa kundi la kutetea haki za binadamu, alipatikana akiwa amekufa katika gari lake karibu na mji mkuu, Kinshasa siku ya Jumatano.

Iliarifiwa kuwa siku hiyo alitarajiwa kukutana na mkuu wa polisi.

Polisi pamoja na kundi aliloongoza Bw Chebeya wamesema mkutao huo haukufanyika.

Mwandishi wa BBC mjini Kinshasa amesema mkuu wa polisi, Bw John Numbi, anaonekana kama mshirika wa karibu wa Rais Joseph Kabila.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu wanasema Bw Chebeya alikuwa akipokea vitisho katika miaka ishirini iliyopita.

Siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alitoa wito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya tukio hilo, huku serikali nayo ikiitisha uchunguzi wake.
Katika taarifa kupitia televisheni, Waziri wa Mambo ya Ndani Adolphe Lumanu alisema Rais Kabila "ananuia ukweli ujulikane" juu ya mauaji ya Bw Chebeya.
"ili kuruhusu uchunguzi ufanyike vizuri, baraza la usalama la taifa liliamua kama hatua ya tahadhari kumsimamisha kazi inspector generali John Numbi," taarifa hiyo ya serikali ilisema.

No comments:

Post a Comment