KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, June 5, 2010

Kifo cha Chebeya chachunguzwa DRC

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametaka upelelezi huru ufanywe nchini Congo kuhusiana na kifo cha mwanaharakati wa haki za binadamu.

Mwili wa marehemu Floribert Chebeya ulipatikana ndani ya gari lake baada ya kuitwa na polisi kwa mkutano ambao baadaye ulisemekana haukufanyika siku ya Jumanne.

Mchunguzi mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyaelezea mazingira ya kifo hicho kama ya kukanganya na yanaonyesha kuhusika kwa vyombo vya dola.

Hata hivyo serikali haijatoa kauli yake ingawa imeitisha uchunguzi ufanywe.

Umoja wa Mataifa una askari wengi wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wanaosaidia nchi hiyo kujikwamua kutoka janga la muda mrefu la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Marehemu Chebeya aliyefariki akiwa na umri wa miaka 47 alikuwa kiongozi wa shirika la kutetea haki za binadamu Voice of the Voiceless na wanaharakati wanasema alikuwa akipokea vitisho kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita.

Mchunguzi mkuu wa upelelezi wa Umoja wa Mataifa Philip Alston alielezea mashaka yake juu ya kifo hicho alipohutubia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva.

Siku ya Alhamisi asubuhi watu wawili kutoka familia ya marehemu huyo, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wanaharakati wawili kutoka shirika la Voice of the Voiceless waliruhusiwa ndani ya chumba cha maiti mjini Kinshasa kuuona mwili wa marehemu.

Waliweza kuona sehemu ya uso kwa sababu sehemu iliyobaki ya mwili ilikuwa imefunikwa shuka ambayo hawakuruhusiwa kuiondoa.

Kabla ya hapo mke wa marehemu alisema kuwa Bw.Chebeya alimpigia simu na kumfahamisha kuwa alikuwa kwenye makao makuu ya polisi kwenye mkutano na mkuu wa polisi na tangu hapo hakusikika tena.

No comments:

Post a Comment