KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, June 24, 2010

Ghana yaiponya Afrika



Aibu iliyokuwa inainyemelea Afrika, ya timu zake zote kukosa kufuzu raundi ya pili ya mashindano ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini ilikatishwa Jumatano baada ya Ghana kufuzu kutoka kundi D.

Ghana ilifuzu licha ya kushindwa 1-0 na Ujerumani, kwa kuwa iliwazidi wapinzani wa karibu katika kundi hilo- Australia kwa wingi wa mabao.

Australia ambayo ilianza michuano hiyo vibaya kwa kufungwa 4-0 na Ujerumani ilijitahidi na kuifunga Serbia mabao 2-0.

Kabla ya mechi hiyo ya Ghana na Ujerumani, vyombo vingi vya habari vya mataifa ya magharibi vilikuwa vinabashiri uwezekano mkubwa wa timu zote za Afrika kuondolewa kwenye hatua za mwanzo, jambo lililoonekana la aibu, kwa kuwa ni mara ya kwanza bara la Afrika linaandaa Kombe la Dunia.
Kevin-Prince Boateng na Jerome Boateng

Kevin-Prince Boateng na kaka yake Jerome Boateng

Ilikuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kwa mchuano kukutanisha ndugu wawili wakichezea timu mbili tofauti. Kevin-Prince Boateng aliichezea Ghana, huku kaka yake Jerome Boateng akiichezea Ujerumani.

Katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg, rangi za bendera ya Ghana zilisheheni kote huku timu hiyo ikitambuliwa kama tumaini pekee la bara Afrika kubakia kwenye mashindano baada ya kuondolewa kwa Cameroon, Afrika Kusini, Nigeria na Algeria.

Ivory Coast ambayo siku ya Ijumaa itachuana na Korea Kaskazini inafahamu vema kwamba kufuzu kwao ni mlima mkubwa sana kwa sababu ni lazima waifunge Korea Kaskazini mabao 8-0 ili kuwapiku Ureno walioinyeshea Korea Kaskazini mvua ya mabao 7-0 siku ya Jumatatu.

Ghana sasa inasubiri kuchuana na Marekani siku ya Jumamosi, kutafuta nafasi ya robo fainali, huku Ujerumani ikichuana na England.

Bao la ushindi la Ujerumani lilifungwa katika dakika ya 60 kwa kwaju la mbali na Mesut Ozil.

Black Stars walionyesha mchezo wa hali ya juu huku mpira wa kichwa wa Asamoah Gyan ukiokolewa karibu na mstari wa lango la Ujerumani na Philip Lahm.

Kwado Asamoah pia aliisumbua ngome ya Ujerumani, na mara mbili mlinda lango wa Ujerumani alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa mikwaju yake.

Ghana itahitaji kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kabla ya kukutana na Marekani , kwani hadi sasa mabao yote mawili waliyofunga kwenye mashindano hayo ya Kombe la Dunia ni kupitia mikwaju ya penalti.

Marekani ilifuzu kutoka kundi C baada ya kuifunga Algeria bao 1-0, bao lilofungwa katika muda wa ziada.

Ushindi huo pia uliiwezesha Marekani kuongoza kundi hilo la C mbele ya England, ambayo iliishinda Slovenia bao 1-0.

Ni mara mbili tu timu za Afrika zimepeta kufika hatua ya robo fainali kwenye Kombe la Dunia.

Mwaka wa 1990 Cameroon ilikuwa nchi ya kwanza kutoka Afrika kufuzu kwa robo fainali, na mwaka 2002 Senegal wakaiga mfano huo.

No comments:

Post a Comment