KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, June 29, 2010

Blatter aomba radhi kwa makosa ya waamuzi


Rais wa shirikisho la soka duniani Sepp Blatter ameomba msamaha kwa ajili ya makosa yaliyofanywa na waamuzi kwenye Kombe la Dunia, ambapo bao llilofungwa na Frank Lampard wa England dhidi ya Ujerumani lilikataliwa, na pia kukubaliwa kwa bao la kuotea lililofungwa na Carloz Tevez wa Argentina dhidi ya Mexico.

Bwana Blatter amesema mdahalo kuhusu haja ya kutumia teknolojia kubaini iwapo mpira umevuka mstari wa goli au la utaanzishwa upya kwenye mkutano wa bodi ya kimataifa ya vyama vya soka utakaofanyika mwezi Julai.

Mkutano wa bodi hiyo uliofanyika mwezi Machi uliamua kukataa kutumika kwa teknolojia hiyo kwenye Kombe la Dunia, kwa tetesi kwamba kusimamisha mechi kwa ajili kuthibitisha kwenye video ikiwa mpira umevuka mstari au la kutaathiri mtiririko wa mchezo na pia kuzinyima timu fursa ya kufunga.

Mjadala kuhusu haja ya kutumika kwa teknolojia hiyo uliibuka tena siku ya Jumapili wakati Ujerumani ilipoifunga England mabao 4-1 mjini Bloemfontein na kuiondoa kwenye mashindano.

Kwenye mechi hiyo, mwamuzi kutoka Uruguay Jorge Larriando na msaidizi wake walikataa kutambua kwamba mpira uliopigwa na Frank Lampard katika dakika ya 38 ulivuka mstari wa lango la Ujerumani na kuingia kabla ya mlinda mlango kuuondosha.

Bao hilo lingeiwezesha England kusawazisha kabla ya mapumziko.

Baadaye siku hiyo katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg kulitokea utata mwingine kwenye mechi kati ya Argentina na Mexico.

Mwamuzi aliruhusu bao la kwanza la Argentina lililofungwa na Carlos Tevez akionekana kuwa ameotea.

Kulitokea mabishano makali uwanjani wakati wa mapumziko baada ya tukio hilo kuonyeshwa tena kwenye skrini kubwa ndani ya uwanja.

Blatter amesema amezungumza na vyama vya soka vya England na Mexico na kuomba msamaha.

No comments:

Post a Comment