KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Thursday, May 6, 2010

Vyama vya wafanyakazi nchini Ugiriki vimeitisha maandamano mapya


Vyama vya wafanyakazi nchini Ugiriki vimeitisha maandamano mapya,siku moja baada ya watu watatu kuuawa katika ghasia zilizozuka wakati wa maandamano ya siku ya Jumatano.

Wakati huo huo, hii leo serikali ya nchi hiyo inaharakisha kupitisha bungeni mpango wa kupunguza matumizi yake. Vyama vikuu vya wafanyakazi vimetoa mwito kwa wanachama wake kuandamana upya, licha ya vifo vitatu vilivyotokea katika tawi la benki ya Marfin iliyotiwa moto na vijana katika mji mkuu Athens, siku ya Jumatano.

Wanawake wawili na mwanamume mmoja waliuawa katika moto huo. Inasemekana kuwa mjaa mzito ni miongoni mwao. Ghasia hizo zilizuka pale watu walipokuwa wakiandamana kupinga hatua kali zinazotazamiwa kuchukuliwa na serikali ili ijiepushe na hatari ya kufiliska. Waandamanaji walijaribu kulivamia bunge na vijana waliojificha nyuso walianza kuchoma moto maduka na mebenki kati kati ya mji mkuu Athens.

Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou amelaani vikali shambulio hilo na akaongezea:

"Kila mmoja ana haki ya kuandamana lakini hakuna mwenye haki ya kuchochea machafuko kama hayo na hasa yakisababisha vifo."

Hata rais wa vyama vya wafanyakazi katika sekta ya binafsi, Carolos Papoulias amekosoa vikali machafuko yaliyotokea hiyo jana lakini amesema kuwa wao wamedhamiria kuendelea na madai yao ya kutaka haki. Amesema, kilicho muhimu hivi sasa, ni kuhifadhi mshikamano na amani katika jamii.Kiasi ya watu 12 walikamatwa na polisi mjini Athens na wengine 37 katika mji wa kaskazini wa Thessaloniki. Huko vile vile waandamanaji walishambulia maduka na mabenki, kabla ya kutawanywa na polisi wa kuzuia ghasia.


Mgomo wa wafanyakazi nchini Ugiriki ni mtihani mkuu wa kwanza kwa jaribio la serikali ya kisoshalisti kupitisha hatua kali za kubana matumizi yake, tangu ilipokubali msaada wa euro bilioni 110 kutoka nchi za kanda inayotumia sarafu ya euro na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF mwishoni mwa juma lililopita. Waziri Mkuu Papandreou amesema, hizo ni hatua zinazopaswa kuchukuliwa na serikali ili kuinusuru nchi yao, lakini hiyo haikusaidia kuzuia maandamano na mgomo uliokwamisha shughuli zote katika sekta za kiserikali zinazohudumia jamii.


Machafuko yaliyozuka mjini Athens yamesababisha wasiwasi mpya katika masoko ya fedha. Inahofiwa kuwa mpango wa serikali unaoazimia kupunguza matumizi yake unaweza kwenda mrama na hivyo mgogoro wake wa fedha huenda ukaziathiri nchi zingine. Hii leo thamani ya hisa katika masoko ya Ulaya imeporomoka vibaya baada ya kupata hasara kubwa hiyo jana. Hata katika masoko ya fedha barani Asia hisa zimeshuka sana.

Miongoni mwa hatua zilizokubaliwa kuchukuliwa na serikali ya Ugiriki juma lililopita, ili kuweza kupata mkopo wa euro bilioni 110 kutoka nchi za kanda ya euro na IMF ni kupunguza mishahara, malipo ya uzeeni, kupandisha umri wa kustaafu na kuongeza kodi ya bidhaa.


Mwandishi: P.Martin/AFPE/RTRE

Mhariri: M.Abdul-Rahman

No comments:

Post a Comment