KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 6, 2010

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.


Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya mgogoro wa Ugiriki.

Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya mgogoro wa Ugiriki unaozidi kuwa mkubwa.

Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya kuapishwa kwa mwislamu wa kwanza kuwa waziri nchini Ujerumani.

Gazeti la Landeszeitung linasema ikiwa dunia ilikuwa inasuburi kupata tahadhari juu ya Ugiriki, basi sasa imetolewa na taasisi ya kutathimini uwezo wa nchi wa kuchukua mikopo.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba dhamana za Ugiriki hazina thamani tena.! Kwa hiyo matumaini yaliyobakia kwa nchi hiyo kabla ya kufilisika ni hatua zitakazochukuliwa na Umoja wa Ulaya pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa mwenye dhima kubwa katika hayo ni kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel aliepaswa kutoa uamuzi mapema badala ya kushughulikia uchaguzi wa jimbo.

Gazeti la Cellesche linailaumu Ugiriki kwa kukosa uadilifu.Gazeti hilo linasema kwamba mwanguko ulishatokea miaka minane iliyopita. Gazeti hilo linaeleza iwapo Ugiriki imefilisika sasa, au zitatumika njia bandia za kurefusha uhai wa mgonjwa huyo, jambo moja ni wazi; kwamba sarafu ya Euro ndiyo inayoathirika. Mhariri wa gazeti la Cellesche Zeitung anasema mambo yalianza miaka zaidi ya minane iliyopita wakati ambapo Ugiriki ilitoa takwimu za uongo ili kuweza kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Gazeti la Bild-Zeitung linatahadharisha kwamba sarafu ya Euro imo hatarini kutokana na mgogoro wa Ugiriki. Kwa hiyo mhariri wa gazeti hilo anasema lazima hatua zichukuliwe ili kuiepusha Euro na hatari ya kuanguka.

Gazeti la Main Post leo linazungumzia juu ya mgogoro unaolikabili kanisa katoliki.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa katika nyakati hizi za mabadiliko duniani, kanisa pia linapaswa pia libadilike.

Waziri wa kwanza mwislamu bibi Aygül Özkan aliapishwa jana katika jimbo la Lower Saxony kaskazini magharibi mwa Ujerumani licha ya zogo kubwa ,kutokana na mwito wake juu ya kupiga marufuku misalaba mashuleni.

Juu mwanasiasa huyo atakaekuwa waziri wa masuala ya kijamii katika serikali ya jimbo hilo, gazeti la Ostsee Zeitung linasema,kauli aliyoitoa itamwandama wakati wote, lakini kutokana na nasaba yake ya uhamiaji , waziri huyo ni tumaini kubwa katika kufanikisha juhudi za kuwaleta pomoja wahamiaji na wajerumani nchini Ujerumani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/ Abdul-Rahman

No comments:

Post a Comment