KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, May 6, 2010

Kocha wa Ujerumani Löw ateua kikosi cha Kombe la dunia 2010


Kombe la Dunia la FIFA likikaribia kuanza mwezi ujao nchini Afrika Kusini,kocha wa Ujerumani Joachim Löw,alitangaza adhuhuri ya leo kikosi chake cha wachezaji 27 ambacho baadae atakipunguza hadi wachezaji 23.

Katika kikosi chake cha makipa 3, Kocha Joachim Löw, ameamua kwa sasa kutomteua nani: kipa nambari 1 langoni kati ya Hans-Joerg Butt wa klabu bingwa Bayern Munich,Manuel Neuer wa makamo bingwa Schalke 04 na Tim Wiese wa Werder Bremen.

Mbali na makipa hao 3,kikosi cha walinzi kinajumuisha Dennis Aogo na Jerome Boateng wote wa Hamburg wenye asili ya kiafrika.Holger Badstuber wa klabu bingwa wa Bayern Munich; Andreas Beck wa Hoffenheim,Arne Friederich wa Hertha Berlin, timu ilioteremshwa daraja ya pili; Per Mertesacker (Werder Bremen); Philip Lahm (Bayern Munich); Serdar Tasci (VFB Stuttgart )na Heiko Westermann wa Schalke 04.

Katika safu ya wachezaji wa kiungo-kikosi cha kati ya uwanja kinaoongozwa na nahodha Michael Ballack (chelsea); Sami Khedira,stadi mwengine wa asili ya kiafrika (Tunisia) Toni Kroos (Bayer Leverkusen) chipukizi Marko Marin na Mesut Ozil wa (Werder Bremen.Kutoka klabu bingwa Bayern Munich, yumo pia hapa Bastian Schweinsteiger; christian Traesch wa Stuttgart na Piotr Trochowski wa Hamburg.

Baada ya kuachwa nje ya kikosi cha washambulizi Kevin kuranyi,alietia jumla ya mabao 18 msimu huu, macho yatakodolewa washambulizi hawa na usoni kabisa ni Miroslav Klose, (Bayern Munich) ambae amewahi kuibuka mtiaji mabao mengi katika Kombe la dunia.Wengine ni Cacu ,msham,bulizi wa asili ya Brazil anaetia mabao kwa Stuttgart.Kuna pia Mario Gomez,Thomas Mueller -wote wa klabu bingwa Bayern Munich.Kikosi hiki cha washambulizi kinakamilishwa na Stefan Kiesling wa Bayer Leverkusen na Lukas Podolski wa FC Cologne.Kutoka Kikosi hiki cha wachezaji 27,kocha Löw atabidi kuchuja tena kabla kuondoka kwa safari ya Afrika kusini ambako Ujerumani imeangukia kundi moja na Australia,Serbia na Black Stars (Ghana).

Kikosi cha Ujerumani, kinaegemea mno wachezaji wengi kutoka Bayern Munich,mabingwa wapya wa Bundesliga na hii inafahamika:kwani, Munich inakaribia kumaliza msimu huu na vikombe 3:Bundesliga,Kombe la klabu bingwa barani Ulaya-(champions League) na Kombe la Taifa la Ujerumani (DFB Pokale).Munich, imefika finali ya vikombe vyote hivyo na Jumamosi hii mjini Berlin, itakabidhiwa Kombe lake la Ligi baada ya firimbi ya mwisho ya mpambano wa mwisho wa msimu na wenyeji-Hertha Berlin.

Wakati lakini Munich , itakuwa ikisherehekea taji lao, wenyeji Hertha Berlin wataweka matanga ya huzuni ya kuteremshwa daraja ya pili.

Ujerumani, itafungua dimba la kundi lake D na Australia,mjini Durban,Juni 13.Kocha Löw, anajua kwamba,nyuma ya mgongo wake, anaandamwa na kivuli cha mshambulizi Kevin Kuranyi,aliemuacha nyumbani. Washambulizi aliowateua wakishindwa kutikisa wavu,basi shoka linamsubiri Löw kumfyeka.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE/SID

Uhariri:Mohammed Abdul-Rahman

No comments:

Post a Comment