KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 10, 2010

Bw Ocampo awasili Kenya


Mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya ICC amewasili Kenya kuchunguza ghasia zilizoibuka nchini humo baada ya uchaguzi.

Zaidi ya watu 1,300 wameuawa na maelfu walihama makazi yao baada ya uchaguzi huo mwaka 2008.

Luis Moreno Ocampo atakutana na watu walioathirika na maafisa wa waandamizi wa serikali katika ziara yake ya siku tano.

Hii ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu majaji wa mahakama hiyo walipompa ruhusa ya kufanya utafiti.

Bw Ocampo, ambaye pia atakutana na mashirika ya kijamii na jumuiya za wafanyabiashara, amependekeza japo watu wawili au watatu washitakiwe.

'Mashahidi kutishiwa'
Baada ya uchaguzi wenye utata wa mwaka 2008, nchi hiyo iligubikwa na ghasia na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa serikalini na wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa kifedha walishutumiwa kwa kuchochea ghasia hizo.

Wanasiasa wa upinzani wametia saini makubaliano ya amani na kukubali kuunda mahakama ya ndani kuchunguza na kwashitaki wahusika.

Lakini mahakama hiyo ya ICC imeingilia kati kutokana na wanasiasa kuzuia uchunguzi kufanyika: mpaka sasa hamna mtu aliyeadhibiwa kutokana na makosa hayo.

Bw Ocampo, aliyeenda Nairobi siku ya Jumamosi, amesema taarifa za mashahidi kutishiwa umezua wasiwasi mkubwa.

Baadhi ya mashahidi wamesema wametishiwa, na wengi wamehamishwa nchini humo kwa usalama wao wenyewe.

Lakini mwendesha mashitaka, anayesema nia kwa ujumla ni kuhakikisha matatizo yaliyoibuka hayajirudii wakati wa uchaguzi mwaka 2012, amesema mashahidi wake watalindwa na ICC.

Bw Ocampo amesema, "Hofu yenu juu ya watu kutishwa kwasababu ni mashahidi umezua wasiwasi mkubwa."

"Lakini tatizo langu ni kwamba siwezi kutoa suluhu kwasababu si wajibu wangu, ni wajibu wa serikali ya Kenya."

Hata hivyo, Bw Ocampo ameliweka wazi kwamba licha ya ICC kutoweza kuwalinda mashahidi wote, mahakama hiyo itakuwa inachukua hatua zake mwenyewe kulinda mashahidi wanaotarajiwa kuitwa.

Amesema, "Mashahidi wangu watalindwa. Tunazungumzia takriban watu 30, 40 au 60."

Awali Bw Ocampo alisema wanasiasa kutoka pande zote mbili wa serikali ya muungano walihusika.

Wakenya wengi wanasubiri kwa hamu majina hayo yatangazwe hadharani, na wana matumaini mashitaka hayo yatasaidia kumaliza mgogoro ulipo nchini humo.

Bw Ocampo kwa sasa bado anategemea zaidi nyaraka zilizofanywa kupitia uchunguzi wa awali. Sasa anahitaji ushahidi wake mwenyewe, na uchunguzi wake utadumu kwa takriban miezi sita.

Wakati mwendesha mashitaka huyo akiendelea na uchunguzi wake, wanasiasa wa Kenya wamelenga zaidi katika masuala yao ya kisiasa. Lakini baadhi huenda wakasimamishwa ghafla na Bw Ocampo.

No comments:

Post a Comment