KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 10, 2010

Hatma ya serikali mpya Uingereza kitendawili


Kiongozi wa chama cha Liberal Democrats, Nick Clegg amekuwa akikutana na wabunge wa chama chake kujadili ombi la kushirikiana na chama cha Conservative katika kuunda serikali mpya ya Uingereza.

Conservative walishinda idadi kubwa zaidi ya viti katika uchaguzi wa Uingereza uliofanyika tarehe 6 Mei, lakini hawakufanikiwa kupata viti visivyopungua 326 ambavyo vingewawezesha kuunda serikali bila kutegemea ushirikiano wa chama au vyama vingine - hali inayomfanya Gordon Brown wa Labour kuendelea kuwa Waziri Mkuu mpaka Conservative watakapounda serikali.

Bw Clegg pia alizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu Brown siku ya Ijumaa. Amesema yuko tayari kuanzisha mazungumzo endapo Lib Dems watashindwa kukubaliana na Conservative.

Siku ya Jumamosi viongozi hao watatu, Bw Clegg, Bw Brown na David Cameron wa Conservative walikutana katika shughuli za kumbukumbu ya kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Kiongozi huyo wa Lib Dem baada ya kukutana na wabunge waandamizi alikuwa azungumze na wabunge wengine aweze kusikia maoni yao, baada ya vyama vyote kukosa uwingi wa viti kuweza kudhibiti bunge.

Matokeo yanaonyesha Conservative walipata viti 306, Labour viti 258, Liberal Democrats viti 57 na vyama vingine vidogo vilivyosalia vinakamilisha orodha katika uchaguzi uliokuwa ukigombania viti 650.

No comments:

Post a Comment